Liverpool safi kwa Wirtz

LIVERPOOL, Mabingwa wa ligi kuu ya England Liverpool FC wamekubali kulipa dau la Euro milioni 116 kumsajili kiungo mshambuliaji wa Ujerumani Florian Wirtz kutoka Bayer Leverkusen. Ada ambayo inajumuisha ‘kishika uchumba’ cha Euro milioni 100 na nyongeza ya Euro milioni 16.
Malipo hayo ya nyongeza yatalipwa ikiwa Liverpool watakuwa na kiwango endelevu cha mafanikio kwenye mashindano makubwa jambo litakalofanya kitita hicho kuwa rekodi ya England. Rekodi ya sasa ya England kwa ada ya awali inasalia kuwa ile ya Chelsea ya Euro milioni 107 kumsajili kiungo wa kati wa Argentina Enzo Fernandez kutoka Benfica mwaka 2023. Na ile ya Moises Caicedo wa Brighton kwa ada ya awali ya Euro milioni 100 ambayo inaweza kupanda hadi euro115 milioni.
Manchester City walikuwa wanamtaka Wirtz kabla ya kujiondoa kwa sababu ya gharama kubwa za dili hilo, Bayern pia wakihusishwa naye. Wirtz alicheza mechi yake ya kwanza akiwa na Leverkusen akiwa na umri wa miaka 17, akifunga mabao 57 katika mechi 197 alizochezea klabu hiyo.
Aliwasaidia kushinda Bundesliga kwa mara ya kwanza mwaka 2024 na amefunga mabao saba katika mechi 31 alizoichezea timu ya taifa ya Ujerumani tangu alipocheza mechi yake ya kwanza kwa taifa hilo mwaka 2021.