Ligi ya wanaume ya Kriketi yazidi kushika kasi

DAR ES SALAAM:LIGI ya TCA Diwa Kriketi wanaume inaendelea kwa kasi huku timu kadhaa zikionesha makali, zikiwemo DIT Gymkhana na MCC ambazo zimeibuka na ushindi muhimu katika michezo mbalimbali iliyopigwa mwishoni mwa wiki.
Katika mchezo wa kwanza, DIT Gymkhana iliichapa Rising Star kwa wiketi 5. Rising Star walifunga alama 39 kwa hasara ya wiketi 8, huku DIT wakijibu kwa kufikisha alama 40 kwa kupoteza wiketi 5 tu.
Katika mechi nyingine, DIT Gymkhana waliendelea kutamba kwa ushindi wa wiketi 3 dhidi ya Pak Stars, ambao walifungwa kwa alama 42. DIT walifikisha alama 43 kwa kupoteza wiketi 7.
MCC walionesha uwezo mkubwa dhidi ya Annadil, wakishinda kwa wiketi 6. Annadil walifunga alama 109 kwa wiketi 8, lakini MCC wakawafikia kwa urahisi kwa kufunga alama 110 kwa hasara ya wiketi 4.
Katika mchezo wa kusisimua, Tanzania Green waliibuka na ushindi wa mikimbio 10 dhidi ya Tanzania Blue, baada ya kufunga alama 127 kwa wiketi 5, na kuizuia Tanzania Blue kufunga zaidi ya alama 117 baada ya kupoteza wiketi zote 10.
K&PA waliitandika vikali Annadil Burhan, kwa ushindi wa mikimbio 90, baada ya kufunga alama 133 kwa wiketi 9, kisha kuwazima wapinzani wao kwa alama 43 pekee kwa kupoteza wiketi zote 10.
RAAH walifanikiwa kuibuka na ushindi wa mikimbio 32 dhidi ya Rising Star, ambapo RAAH walifunga alama 78 kwa wiketi 5, huku Rising Star wakifunga alama 46 kwa wiketi 6 tu katika muda uliowekwa.
Katika mchezo mwingine, 3D waliwazidi nguvu Wicked Wackers, kwa ushindi wa mikimbio 32 baada ya kufunga alama 93 kwa wiketi 3, na kuizuia Wicked Wackers kufunga zaidi ya alama 61 kwa wiketi 5.
Unisoft Aces C waliibuka na ushindi wa wiketi 5 dhidi ya Tamil Nadu Sports, baada ya kuwazuia wapinzani wao kwa alama 67 na kufunga alama 68 kwa kupoteza wiketi 5 pekee.
Katika mchezo wa mwisho, Lions B waliwafunga Estim A kwa ushindi wa wiketi 8. Estim walifunga alama 114 lakini Lions B wakawafikia kwa kufunga alama 110 kwa hasara ya wiketi 2 tu.