
MOROGORO: MWIMBAJI wa muziki wa Injili anayekuja kwa kasi kutoka mkoani Morogoro, Lazaro Suda, amewaomba wadau na mashabiki wa muziki huo kuupokea kwa mikono miwili wimbo wake mpya unaoitwa “Maadui”, ambao amesema una ujumbe mzito unaogusa jamii.
Suda amesema dhamira yake kubwa ni kuitangaza Injili ya Yesu Kristo, huku akiitambulisha Morogoro kama moja ya ngome mpya ya vipaji vya muziki wa Injili nchini, jambo linalompa motisha ya kuendelea kuachia nyimbo zenye mguso wa kipekee.
Akizungumza na SpotiLeo, Suda amesema wimbo “Maadui” tayari umewekwa kwenye chaneli yake ya YouTube, akieleza matumaini yake kuwa ujumbe uliobebwa ndani ya wimbo huo utawafikia watu wengi bila kujali tofauti zao.
“Mungu amenituma kwa sasa nimtangaze hapa Morogoro kupitia muziki. Ndiyo maana nimeendelea kutoa nyimbo zenye ujumbe wa kipekee unaojenga jamii. Naomba watu wote, bila kujali dini zetu, wasikilize wimbo huu, kuna jambo muhimu tutajifunza,” amesema Suda.
Ameongeza kuwa wimbo huo unawahimiza watu kuwa imara katika imani, kuvumilia changamoto na kuendelea kumtegemea Mungu hata wanapokutana na vikwazo kutoka kwa maadui wa maendeleo yao.
Kwa hatua hiyo, Lazaro Suda anaendelea kujijengea jina katika muziki wa Injili, huku akisisitiza kuwa muziki ni chombo cha mabadiliko chenye uwezo wa kuleta matumaini na faraja kwa jamii.




