Muziki

Lady JayDee amesema umri si kikwazo cha kupendeza

DAR ES SALAAM: Msanii wa Bongo Fleva, Judith Wambura ‘Lady JayDee’, amezungumzia mabadiliko ya mwili yanayokuja kadri umri unavyosonga, huku akisisitiza kuwa hilo halitamzuia kuendelea kupendeza na kufurahia maisha.

Kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii, Lady JayDee ameandika kuwa kuna wakati unafika mambo ya kubana tumbo hayawezekani tena, na badala yake mtu anatakiwa kuukubali mwili wake ulivyo.

“Kuna umri ukifika kumbe hata kulibana tumbo inakuwa haiwezekani tena, basi wacha lielee elee tu,” ameandika.

Msanii huyo pia amegusia suala la kuzeeka akieleza kuwa ni baraka kuishi miaka mingi, huku akiwataka watu kuacha kuwahukumu au kuwadhihaki wanaozeeka.

“Baraka ni kuishi miaka mingi duniani. Endapo unateseka na umri mkubwa wa mtu basi nikuombee Mungu akupumzishe ukiwa na miaka 20 ili umri usije ukakutesa,” ameongeza.

Katika kauli yake iliyovutia wengi, Lady JayDee amesisitiza kuwa yeye na wenzake wataendelea kufurahia maisha bila kujali umri wao.

“Sisi bado tunaendelea kunywa wine na kuvaa crop tops hadi tufikishe miaka 90,” amesema kwa kujiamini.

Baadhi ya mashabiki wamepongeza ujasiri wake wa kuhimiza kukubaliana na hali kwa mabadiliko ya mwili na kujiamini, huku wengine wakijadili nafasi ya fasheni katika umri tofauti.

Related Articles

Back to top button