Muziki

Lady Jaydee aingia mkataba mkubwa na Universal Music Group East Africa

DAR ES SALAAM:MSANII mkongwe wa muziki wa Bongo Fleva, Judith Wambura maarufu kama Lady Jaydee, amepata dili kubwa baada ya Kampuni ya Universal Music Group East Africa kutangaza rasmi ushirikiano wake na nyota huyo wa Afrika Mashariki.

Lady Jaydee anatambulika kama mmoja wa wasanii wenye sauti yenye ushawishi mkubwa na iliyodumu kwa muda mrefu katika tasnia ya muziki wa ukanda huu, hatua inayofanya ushirikiano huo kuwa wa kihistoria.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa, ushirikiano huo unaakisi imani ya pamoja juu ya nguvu ya muziki wa Afrika Mashariki pamoja na wajibu wa wasanii wakubwa katika kuukuza na kuufikisha katika soko la kimataifa.

Hatua hiyo pia imeelezwa kuwa ni sehemu muhimu ya mkakati wa Universal Music Group East Africa wa kuibua na kukuza vipaji bora zaidi kutoka katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Kupitia makubaliano hayo, pande zote zimejipanga kuinua ubora wa muziki, kupanua wigo wa usikivu duniani na kuimarisha nafasi ya muziki wa Afrika Mashariki katika jukwaa la kimataifa.

Universal Music Group East Africa imeeleza furaha yake kufanya kazi na wasanii wenye maono, uzoefu na dhamira ya ubora, ikibainisha kuwa uwepo wa Lady Jaydee katika ushirikiano huo ni heshima kwa mchango wake mkubwa katika muziki, huku pia ukiwa mwanzo wa safari mpya yenye mafanikio makubwa.

Related Articles

Back to top button