Michezo Mingine

Kriketi kusaka tiketi ya Kombe la Dunia

DAR ES SALAAM: KIKOSI cha Taifa cha Wanaume cha Kriketi Tanzania (Men’s T20) kiko kwenye maandalizi ya mwisho kuelekea Harare, Zimbabwe, kushiriki Fainali za Kanda ya Afrika za Kufuzu Kombe la Dunia la Kriketi T20 la ICC 2025 zitakazofanyika kuanzia Septemba 26 hadi Oktoba 4 mwaka huu.

Kwa mujibu wa taarifa ya Chama cha Kriketi Tanzania, mashindano hayo yanatoa nafasi ya kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia, hivyo wachezaji wa Tanzania wamejikita vilivyo katika mazoezi kuhakikisha wanapigania bendera ya taifa kwa nguvu zote.

Ratiba ya mechi za awali inaonesha Tanzania itaanza kampeni zake kwa kuvaana na Botswana Septemba 26 Takashinga Cricket Club. Baada ya hapo, vijana hao watachuana na Uganda Septemba 28, kabla ya kukutana na wenyeji Zimbabwe Septemba 30 kwenye Uwanja wa Harare Sports Club.

Iwapo Tanzania itafanya vizuri, itapata nafasi ya kucheza nusu fainali Oktoba 2 na baadaye fainali Oktoba 4, ambazo ndizo zitakazoamua timu zitakazofuzu Kombe la Dunia.

Nahodha wa kikosi hicho, Kassim Chete, ameahidi kuongoza wenzake kwa nidhamu na ari kubwa akisema kila mchezaji anaelewa jukumu lake.

“Tunapiga hatua kila siku, kila mpira na kila mazoezi ni maandalizi ya kutupeleka Kombe la Dunia. Hii siyo safari ya kawaida, ni safari ya kupeperusha bendera ya Tanzania duniani,” alisema.

Kwa sasa kikosi hicho kimejikita katika mazoezi ya mbinu, uimara wa mwili na mshikamano wa timu, kuhakikisha kuwa kila mchezaji yupo tayari kwa mapambano makubwa.

Watanzania wanahimizwa kuungana na kikosi hiki kwa sala na dua, sambamba na kutoa hamasa kupitia mitandao ya kijamii ili kuongeza nguvu ya morali kwa wachezaji wanaoelekea Zimbabwe.

Related Articles

Back to top button