Kombe la Dunia la Klabu timu 32
						SHIRIKISHO la Kimataifa la Mpira wa Miguu(FIFA) limetangaza kuanzishwa kwa michuano mipya ya Kombe la Dunia la Klabu itakayoshirikisha timu 32.
Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari mjini Doha, Qatar kuelekea fainali ya Kombe la Dunia 2022 Desemba 17 Rais wa FIFA Gianni Infantino amesema michuano hiyo mipya itaanza mwaka 2025.
Kombe la Dunia la Klabu la Wanawake pia litaanzishwa huku ikithibitishwa pia kuwa Kombe la Dunia la Klabu 2022 kwa wanaume litafanyika Morocco kati ya Februari mosi na 11, 2023 likishirikisha timu saba kama ilivyo kawaida kwa sasa.
FIFA ilianzisha Kombe la Dunia la Klabu 2000 na limekuwa likishindaniwa na timu saba katika msimu 14 kati ya 15 iliyopita huku mshindi wa Ligi ya Mabingwa ulaya akiingia hatua ya nusu fainali.
Kombe hilo hushindaniwa na washindi wa Ligi ya Mabingwa Asia, Ligi ya mabingwa Afrika, Ligi ya mabingwa amerika ya Kaskazini, kati na Caribbean, Ligi ya Mabingwa Amerika Kusini, Ligi ya Mabingwa Oceania na mshindi wa msimu uliotangulia wa Ligi ya Mabingwa Ulaya pamoja na Bingwa mtetezi wa taifa mwenyeji.
Hata hivyo klabu kadhaa kubwa barani ulaya zimepinga mapendekezo ya kuanzishwa michuano hiyo mipya ya Kombe la Dunia la Klabu.
				
					



