Koeman aendelea kukoleza moto wa Depay

EUROBORG:KOCHA wa timu ya taifa ya Netherland Ronald Koeman amesema kitendo chake cha kumtoa Mshambuliaji Memphis Depay ni kumfanya mchezaji huyo kuwa na njaa zaidi ya mabao baada ya Depay kunyimwa nafasi ya kukamilisha hat-trick na kujiweka juu ya ‘listi’ ya wafungaji wa muda wote wa timu ya taifa hulo maarufu la soka Duniani.
Depay alifunga mabao mawili ndani ya dakika 16 za mwanzo katika mchezo ambao Netherlands walipata ushindi mnono wa mabao 8-0 mbele ya timu ya taifa ya Malta katika mechi ya kufuzu Kombe la Dunia 2026 na kufikia rekodi ya Robin van Persie mwenye mabao 50 huku wachezaji wote wawili wakiwa na mabao 50 katika mechi 102 za kimataifa.
Akizungumza na kituo cha Televisheni cha taifa hilo kocha Koeman amesema siku zote amekuwa akiamini kuwa Depay ni mchezaji mzuri na anastahili pongezi baada ya kurejea kutoka majeruhi na kufanya vizuri huku akisema kumtoa wakati ambao angeweza kuipiku rekodi ya Van Persie likuwa ni kumfanya awe na njaa zaidi ya kufunga.
“Siku zote nimekuwa nikidhani Memphis ni mchezaji mzuri. Nadhani anastahili pongezi kubwa. Amekuwa na mwaka mzima wa majeraha, lakini yuko fiti na ana njaa ya kufunga sasa. Ni vizuri kwamba hakufunga la tatu, kwa sababu njaa yake itaendelea na atalitafuta bao hilo kwa nguvu.” alisema Koeman.
Kwa upande wake Depay alisema amefurahishwa na kitendo chake cha kusawazisha idadi hiyo ya mabao huku akisema ni suala la muda tu na anaamini ikiwa kocha Koeman atamuamini na kumpa nafasi zaidi atafanya maajabu.
“Nimesawazisha rekodi ya Van Persie, nimefurahi. Lakini hii ni namba ya muda tu. Bila shaka ninaendelea na 51, 52 na 53. Kama ningecheza muda mrefu zaidi, ningefunga moja zaidi usiku wa leo,” alisema Depay, ambaye alitolewa dakika ya 72 timu yake ikiwa mbele kwa mabao 4-0.
Depay alifunga bao lake la kwanza la kimataifa dhidi ya Australia kwenye Kombe la Dunia la 2014 nchini Brazil lakini si mara zote imekuwa rahisi kwake kwa miaka mingi akiwa na timu ya taifa. Na sasa yuko kwenye moto wa kuipeleka Netherlands kwenye fainali za mwakani nchini Marekani, Mexico na Canada.