Kocha Simba ampa heko Mpanzu

SINGIDA: KOCHA Mkuu wa Simba Steven Barker amesema haikuwa rahisi kwa Simba kupata ushindi dhidi ya Singida Black Stars katika mchezo wa Ligi Kuu uliochezwa kwenye Uwanja wa Airtel, lakini juhudi na mapambano ya wachezaji hadi dakika za mwisho yaliwapa ushindi wa mabao 2-1.
Akizungumza baada ya mchezo huo, Barker, amesema ulikuwa mchezo mgumu na wenye changamoto kubwa, lakini wachezaji wake walionesha tabia ya kupambana na kuendelea kuamini hadi wakapata bao la ushindi katika dakika za mwisho.
Barker amesema katika soka wakati mwingine ushindi hupatikana mwishoni mwa mchezo, hivyo aliwataka wachezaji wake kuendelea kupambana bila kukata tamaa hadi dakika za mwisho.
“Unajua wakati mwingine ni lazima uendelee kufanya kazi kwa bidii, kusukuma mbele na kuamini. Wakati mwingine mechi hushindwa au kushindwa katika dakika za mwisho kama ilivyokuwa leo (Jana),” amesema Barker.
Ameongeza kuwa wachezaji wake walionesha moyo mkubwa wa kujituma na uthabiti licha ya presha ya mchezo huo.
“Ulikuwa mchezo mgumu kwetu, lakini wachezaji walionyesha tabia kubwa ya kupambana, kujituma na kuendelea kuamini hadi mwisho,” amesema.
Barker pia alimpongeza kiungo Mpanzu kwa kuingia akitokea benchi na kufunga bao la ushindi lililoihakikishia Simba pointi tatu muhimu.
“Niliwaambia wachezaji kwamba mechi huchezwa hadi dakika ya 95 au 96, hivyo ni lazima kuendelea kupambana hadi mwisho. Ni vizuri kuona Mpanzu aliingia na kufunga bao la ushindi,” amesema.




