Kwingineko

Kocha Martinez: Kadi nyekundu ya Ronaldo ni ya kikatili

DUBLIN: KOCHA wa timu ya Taifa ya Ureno, Roberto Martinez, amesema kadi nyekundu aliyopewa nahodha wake Cristiano Ronaldo ilikuwa ya kikatili na kali mno, baada ya mshambuliaji huyo kutolewa nje kwa mara ya kwanza katika mechi za kimataifa wakati Ureno ikilala mabao 2-0 dhidi ya Ireland kwenye mechi ya kufuzu Kombe la Dunia, Alhamisi usiku jijini Dublin.

Awali Ronaldo alipewa kadi ya njano kwa kumpiga kiwiko beki Dara O’Shea, lakini baada ya kupitia VAR adhabu hiyo ikabadilishwa na kuwa kadi nyekundu. Ilikuwa mara yake ya kwanza kutolewa nje katika mechi 226 alizocheza kwa timu ya taifa.

“Niliiona kama adhabu kali kwa sababu anajali timu. Alikuwa zaidi ya dakika 60 akivutwa, kusukumwa, kushikwa, na akaonekana tu akijaribu kujinasua. Nadhani tukio linaonekana baya kuliko lilivyokuwa. Sio kama amempiga kiwiko, ni mwendo wa mwili mzima, lakini kamera inaifanya ionekane kama kiwiko. Lakini tumekubali uamuzi.” – Martinez aliwaambia waandishi wa Habari.

Martinez pia alijibu kauli za kocha wa Ireland, Heimir Hallgrimsson, aliyedai kuwa Ronaldo alikuwa na udhibiti waamuzi kwenye mechi ya kwanza jijini Lisbon, ambayo Ureno ilishinda 1-0.

“Kitu pekee kilichoniacha na ladha mbaya ni kocha wa Ireland jana kuongelea suala la waamuzi kuathiriwa na uwepo wa Ronaldo. Kisha leo, beki mkubwa anaanguka chini kwa njia ya kusisimua sana kutokana na mgeuko wa mwili wa Cristiano” – amesema Martinez.

Ureno, ambao tayari wamehakikisha angalau nafasi ya mtoano, wanaongoza Kundi F kwa pointi mbili mbele ya Hungary kwa tofauti bora ya mabao, huku Ireland wakifuatia kwa pointi moja nyuma.

Katika mechi za mwisho Jumapili, Ureno wataikaribisha Armenia, huku Ireland wakisafiri kuivaa Hungary.

Related Articles

Back to top button