Habari Mpya

KMC yadondosha balaa NBCPL, yashusha Mcameroon

DAR ES SALAAM: Watoza ushuru wa manispaa ya Kinondoni KMC FC, wamekamilisha usajili wa mshambuliaji Austin Ajoh kutoka klabu ya Union Sportive ya Cameroon kwa mkataba wa miaka miwili kuanzia msimu wa 2024/25.

Ajoh anakuja kuchukuwa nafasi ya Waziri Junior, kinara wa kufumania nyavu wa kikosi hicho ambaye ameaga rasmi na msimu ujao hatakuwa sehemu ya kikosi cha timu hiyo.

Akizungumza na Spotileo, Msemaji wa KMC FC, Khalid Chukuchuku amesema usajili ya mshambuliaji huyo ni kuimarisha eneo la ushambuliaji kurithi nafasi ya Waziri Junior.

Amesema wamefanikiwa kumsajili mchezaji huyo kutoka Union Sportive ya Cameroon ikiwa ni mapendekezo ya benchi la ufundi katika kuimarisha kikosi chao kwenye safu ya ushambuliaji.

“Tumekamilisha usajili wa nyota huyo, bado mchakato wa usajili unaendelea kwa kufuata mapendekezo ya kocha Abdihamid Moallin, kufanya maboresho katika kila eneo la timu yetu,” amesema Khalid.

Amesema baada ya kufanya usajili wa kipa kutoka Burundi na leo mshambuliaji huyo wanaendelea na mchakato wa kukamilisha sajili kabla ya wiki ijayo ambayo wanatarajia kwenda visiwani Zanzibar kwa ajili ya kambi.

KMC FC imekamilisha usajili wa wachezaji sita kwenye dirisha kubwa la usajili akiwemo Ajoh, Fabien Mutombora (Kipa), Oscar Paul (Mshambuliaji), Nicky Kassami, Jean Nyezimana na Salum Stoper

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button