Kifo cha Boupendza chawaibua mashabiki China

HANGZHOU: Mashabiki wa soka nchini China wameonesha kasirishwa na uamuzi wa Zhejiang FC kuendelea na mechi ya ligi saa chache baada ya kifo cha mshambuliaji wao wa kimataifa wa Gabon Aaron Boupendza aliyefariki baada ya kuanguka kutoka ghorofa ya 11 ya jengo alilokuwa akiishi jana Jumatano.
Mashabiki wa klabu hiyo yenye maskani yake mjini Hangzhou walitumia mitandao ya kijamii kulaani kitendo cha Zhejiang FC kucheza mechi katika uwanja wa nyumbani ya Ligi Kuu ya China (Chinese Super League) dhidi ya Meizhou Hakka, huku wengi wakitarajia mchezo huo kusogezwa mbele ili kuipa nafasi klabu na mashabiki kuomboleza kifo cha mshambuliaji wao.
“Kwani mechi hii haikupaswa kuahirishwa?” shabiki mmoja aliandika kwenye mtandao wa kijamii wa Weibo ambao unafanana na ule wa X zamani twitter. “Kwanini hawakuahirisha mchezo huu? Kweli ligi ya China ni ya chini sana” mwingine aliandika katika mtandao wa WeChat
Mechi hiyo iliyomalizika kwa sare ya 2-2, ilichezwa katika hali ya ukimya huku kukiwa hakuna mchezaji yeyote wa kigeni wa klabu hiyo aliyeingia uwanjani. Mashabiki waliimba jina la Boupendza, na kuinua shati lake na kuwasha tochi za simu, na baada ya filimbi ya mwisho wachezaji na wafanyakazi wa Zhejiang FC walienda kwa mashabiki kama kitendo cha maombolezo ya pamoja.
Nahodha wa Zhejiang fc Cheng Jin alijitahidi kujibu maswali ya waandishi wa Habari baada ya mechi lakini alikatisha mahojiano baada ya kushindwa kusema chochote kutokana na huzuni. Kocha wa kikosi hicho pia Mhispania Raul Caneda Perez alisema hana la kusema kuhusu mchezo na kuongeza kuwa haikuwa siku sahihi ya kuongelea soka.
Polisi wa Hangzhou walithibitisha kifo cha Boupendza huku wakisema hakuna dalili za kutendeka jinai yeyote baada ya uchunguzi ambao ulijumuisha mahojiano na mashuhuda Pamoja na video za kamera za CCTV.
Boupendza alifikwa na umauti hospitalini, baada ya juhudi za kupambania uhai wake kutofua dafu. Zhejiang FC ilitoa taarifa kuhusu kifo cha Boupendza baada ya mechi na kusema wanashirikiana kikamilifu na mamlaka husika kufanya uchunguzi.