Kapombe: Hatutishiki,Amaan Kama Mkapa

ZANZIBAR: BEKI wa klabu ya Simba, Shomari Kapombe, amesema mabadiliko ya uwanja wa mchezo wa marudiano wa fainali ya Kombe la Shirikisho la CAF dhidi ya RS Berkane hayajaathiri kabisa maandalizi yao kuelekea mechi hiyo muhimu.
Awali, pambano hilo lilipangwa kufanyika kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, lakini baadaye Shirikisho la Soka Afrika (CAF) lilielekeza mechi hiyo kuchezwa New Amaan Complex, Zanzibar – jambo lililoibua hisia mseto kutoka kwa mashabiki.
Hata hivyo, Kapombe amesema wachezaji wa Simba wapo tayari kwa ajili ya mapambano na wanauchukulia Uwanja wa New Amaan kama nyumbani kwao vilevile.
“Kama vile tunapokuwa Uwanja wa Benjamin Mkapa, ndivyo tutakavyokuwa hapa Zanzibar. Tunahitaji kupeperusha bendera ya Tanzania ambayo tumeibeba,” amesema.
Simba inakabiliwa na kazi kubwa ya kuifunga RS Berkane kwa mabao 3-0 ili kufuta kichapo cha mabao 2-0 walichopokea kwenye mechi ya kwanza iliyopigwa nchini Morocco.
Kapombe amesema wachezaji wanatambua uzito wa mechi hiyo, wakijua pia kuhusu historia ya soka ya Tanzania, hususan mwaka 1993 ambao umekuwa kumbukumbu muhimu kwa mashabiki.
“Tunaenda kufanyia kazi maelekezo ya benchi la ufundi. Mwaka 1993 wengine hatujazaliwa au tulikuwa wadogo, lakini historia ipo. Tupo tayari kwa ajili ya mchezo huu na kupambania hisia za Watanzania,” ameongeza Kapombe.