Kane kutua Bavaria kwa bil 291/-

MABINGWA wa Ujerumani Bayern Munich imekubaliana kimsingi na Tottenham Hotspur ada ya pauni milioni 95 sawa na shilingi bilioni 291.5 kwa ajili ya uhamisho wa Harry Kane.
Klabu hizo zimekuwa katika mazungumzo kwa wiki kadhaa kuhusu uhamisho wa muda mrefu wa Kane kwenda Munich.
Sasa Kane mwenye umri wa miaka 30 ana uamuzi wa kufanya iwapo anataka kwenda Ujerumani huku kukiwa na ongezeko la hisia nahodha huyo wa England anaegemea kubaki Spurs.
Ofa ya tatu ya Bayern ya pauni milioni 86 iliyowasilishwa wiki iliyopita ilitupwa.
Hata Hivyo, ofa iliyoboreshwa inasemekana kuwa karibu na aliyohitaji Mwenyekiti wa Tottenham, Daniel Levy kumnunua Kane.
Levy anaona thamani ya Kane ni pauni milioni 120 lakini vyanzo vya habari vya kuaminika vinaonesha ofa inayokaribia pauni milioni 100 itaishawishi klabu hiyo kumuuza mchezaji huyo ambaye majira yajayo ya joto atakuwa huru.
Kane anataka hatma yake ipatiwe ufumbuzi mwisho wa wiki hii na hatatafakari uhamisho mara baada ya Ligi Kuu England kuanza Agosti 11.
Sasa Bayern ya Jimbo la Bavaria italazimika kutimiza masharti yote yanayotakiwa kumhamisha Kane ambaye awapo itamsajili atakuwa akilipwa pauni milioni 400,000 sawa shilingi bilioni 1.2 kwa wiki.