Kamwe: Yanga haijengi timu, inaboresha kikosi

DAR ES SALAAM: OFISA Habari wa Klabu ya Yanga, Ali Kamwe, ameweka bayana kuwa klabu hiyo haipo katika hatua ya kujenga kikosi kipya, bali inaendelea na mchakato wa kuboresha timu iliyopo tayari ili kuimarisha ushindani kwenye mashindano ya ndani na nje ya nchi.
Kauli hiyo ya Kamwe imekuja kufuatia taarifa na tetesi zilizoenea mitandaoni kuwa Yanga imepanga kusajili idadi kubwa ya wachezaji msimu huu, jambo lililoibua hofu kwa baadhi ya mashabiki wakihofia kuwa huenda msingi mzuri wa timu ukaanza kuvunjwa.
Kamwe amesema msimu uliopita Yanga ilikuwa na kikosi bora kilichotoa upinzani mkali kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara pamoja na michuano ya kimataifa, hivyo si sahihi kuamini kuwa klabu hiyo inaanza upya.
“Tunachofanya sasa ni kuboresha pale palipoonekana kuwa na mapungufu. Yanga haijengi timu mpya, bali inaimarisha ile iliyopo,” amesema.
Ameeleza kuwa lengo kubwa la maboresho hayo ni kumpa kocha mpya wachezaji wanaoendana na falsafa yake ya soka la pasi nyingi, kasi, uchezaji wa kuvutia, akisisitiza kuwa mfumo huo hautapotea kwani ndio unaoleta matokeo chanya.
Kwa mujibu wa Kamwe, baadhi ya wachezaji walioonesha kiwango bora msimu uliopita wataendelea kubaki klabuni, huku usajili unaoendelea ukilenga kuongeza ubora zaidi na kuzingatia mahitaji ya kisasa ya mchezo wa soka unaohitaji wachezaji wenye kiwango cha juu kimataifa.
“Kwa ujumla, Yanga haitafanya mabadiliko makubwa katika kikosi chake, bali itafanya usajili wa kimkakati wenye lengo la kufanikisha azma ya kufanya vizuri zaidi katika mashindano ya kimataifa, hususan Ligi ya Mabingwa Afrika,” amesema Kamwe.