Job awapa ujumbe mzito Yanga Princess

DAR ES SALAAM: KATIKA hafla ya kipekee ya utoaji wa tuzo kwa wachezaji wa Yanga Princess waliofanya vyema msimu huu, beki tegemeo wa kikosi cha wanaume cha Yanga SC, Dickson Job, aliibuka na ujumbe mzito wa matumaini na hamasa kwa timu hiyo ya wanawake.
Amesema kuwa tuzo hizo si tu kutambua juhudi za wachezaji hao, bali ni chachu ya mabadiliko makubwa ndani ya kikosi hicho kinachozidi kuonesha ukuaji kila msimu.
“Lazima tuandike historia mpya kuanzia sasa. Wanatakiwa kuendeleza walipoishia kwa nguvu na juhudi zaidi. Walichokifanya msimu huu ni zaidi ya matokeo; ni dira ya mafanikio yajayo,” amesema
Licha ya Yanga Princess kumaliza katika nafasi ya tatu kwenye Ligi Kuu ya Wanawake Tanzania, nyuma ya Simba Queens na mabingwa watetezi JKT Queens, Job amesisitiza kuwa mafanikio hayo ni ishara ya timu inayokua na yenye uwezo wa kutwaa ubingwa katika siku za usoni.
“Nawapongeza kwa moyo mmoja. Wamepambana, wameonyesha dira. Kwa kile walichokifanya msimu huu, naamini ni mwanzo wa safari ya mafanikio makubwa,” ameongeza.
Job amewapongeza kocha mkuu wa Yanga Princess, Enda Lema, kwa kazi kubwa ya kuunda kikosi imara licha ya changamoto za mabadiliko ya wachezaji msimu huu.Amesema kuwa mafanikio ya timu hiyo ni matokeo ya mshikamano, nidhamu na mbinu bora za ukocha.
“Ni mara ya kwanza kwa timu ya wanawake ya Yanga kutambuliwa rasmi kwa namna hii. Hata sisi timu ya wanaume hatujawahi kufanyiwa hafla ya aina hii. Hii ni njia sahihi ya kujenga ari na morali kwa wachezaji wetu,” amesema.
Job amewataka wachezaji wa Yanga Princess kuendelea kujituma na kuto kata tamaa, huku akisisitiza kuwa ndoto ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Wanawake kwa mara ya kwanza katika historia ya klabu hiyo ipo ndani ya uwezo wao.