JKT Queens yarudia enzi zake

JINA la JKT Queens kwenye soka la wanawake Tanzania Bara lina historia ndefu.
Timu hii ilianza kucheza Ligi ya Wanawake wakati ikichezwa Mkoa wa Dar es Salaam pekee ikiwa pamoja na Sayari Women, Mburahati Queens, Emima, Kiwohede, Kilimanjaro Queens
na nyingine ambazo hazipo ama zinacheza ligi za chini.
Hata hivyo, katika majina ya timu za zamani za wanawake ambazo zinaendelea vizuri na
zimeandika historia ya kutwaa mataji ni JKT Queens pekee waliofanikiwa kufikia rekodi ya
Simba Queens ya kutoa ubingwa mara tatu.
UBINGWA
JKT Queens ambayo inamilikiwa na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) Makao Makuu Mlalakuwa
ambapo sasa yamehamia Dodoma, ilitwaa ubingwa wake wa kwanza msimu wa mwaka
2017-18 ikiwavua mabingwa wa kihistoria, Mlandizi Queens ambao ni mabingwa wa kwanza tangu Ligi Kuu ya wanawake kuanzishwa.
Msimu uliofuata wa mwaka 2018-19 ilitetea ubingwa wake na baada ya hapo haikufanya vizuri hadi iliporudi msimu huu wa 2022-23 na kufanikiwa kutwaa ubingwa bila kufungwa.
JKT Queens imechukua ubingwa huo na kumaliza utawala wa Simba Queens ambayo
iliuhodhi kwa misimu mitatu mfululizo.
Simba Queens iliukosa ubingwa kwa kushindwa kuifunga JKT Queens msimu huu, mechi ya kwanza ilifungwa mabao 2-1, kwenye Uwanja wa Mo Arena, Dar es Salaam na waliporudiana walitoka sare ya bao 1-1, mechi ikichezwa Uwanja wa Meja Jenerali, Isamuhyo, Mbweni, Dar es Salaam.
Kikosi cha JKT Queens kilichotwaa ubingwa msimu huu asilimia kubwa ndicho kikosi kilichotwaa ubingwa msimu wa 2017-18 na 2018-19 na baadaye wengi wakakimbia timu hiyo, lakini wamerudi sasa wakiwa ndani ya gwanda wakiwa waajiriwa wa JKT.
KIMATAIFA
Kwa ubingwa huo, sasa JKT Queens itaiwakilisha Tanzania kwenye michuano ya Afrika Mashariki na Kati (Cecafa) itakayofanyika kuanzia Juni 3-17, mwaka huu huko Kenya ili kusaka mwakilishi wa ukanda huu atakayekwenda katika michuano ya Ligi ya Mabingwa
Afrika.
Pia JKT Queens inatarajiwa kuiwakilisha Tanzania katika mashindano ya kuwania ubingwa wa majeshi wa dunia kwa wanawake (World Military Women Football Championship)
nchini Uholanzi.
Kutokana na jukumu hilo la kitaifa, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Innocent Bashungwa amewataka mashabiki wa Simba na Yanga kuiunga mkono timu hiyo.
MFUNGAJI BORA
Mfungaji bora ni Jentrix Shikangwa mwenye mabao 17 wa Simba Queens. Shikangwa ambaye alisajiliwa katika dirisha dogo la usajili Desemba, mwaka jana amekuwa msaada
mkubwa kwenye timu yake iliyomaliza nafasi ya pili baada ya kufikisha pointi 45, moja pungufu dhidi ya mabingwa, JKT Queens.
Mchezaji huyo anafuatiwa na Winfrida Charles wa Alliance Girls ya Mwanza ambaye amefunga mabao 13, Donisia Minja wa JKT Queens mwenye mabao 12 anashika nafasi ya tatu akifuatiwa na Stumai Abdallah wa JKT Queens pia mwenye mabao 10.
NAFASI NYINGINE
Baada ya bingwa JKT Queens na mshindi wa pili Simba Queens nafasi ya tatu imechukuliwa na FountainGate Girls, Yanga Princess wanashika nafasi ya nne, Alliance Queens inashika
nafasi ya tano, Ceasiaa Queens ni ya sita, Baobab Queens inashika nafasi ya saba na Amani Queens inashika nafasi ya nane ya tisa Mkwawa Queens na The Tigers Queens.
ZILIZOSHUKA
Mkwawa Queens na The Tigers Queens zimeshuka daraja rasmi na msimu ujao zitakuwa zikicheza Ligi ya Championship.
ZILIZOPANDA
Timu za Geita Queens na Bunda Queens zimepanda Ligi Kuu ya wanawake kwa msimu ujao kujaza nafasi za Mkwawa Queens na The Tigers Queens ambazo zimeshuka daraja.