Jesus mambo safi UCL

BRUGES: KOCHA wa Arsenal Mikel Arteta amesema mshambuliaji wa klabu hiyo Gabriel Jesus anaweza kurejea katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya leo Jumatano baada ya kukosekana kwa muda mrefu, lakini atawakosa tena nyota kadhaa muhimu akiwemo Declan Rice na Leandro Trossard.
Mshambuliaji huyo wa Brazil amekuwa nje tangu Januari baada ya kupata jeraha la mshipa wa goti (ACL) kwenye mechi ya Kombe la FA dhidi ya Manchester United. Alirejea mazoezini mwezi uliopita na amekuwa mchezaji wa akiba asiyeingia uwanjani dhidi ya Chelsea na Brentford katika wiki za karibuni.
Arteta amesema awali walitarajia Jesus kuanza mazoezi mwezi huu, lakini mshambuliaji huyo alionesha kasi ya ajabu kwenye kupona kwake hali iliyoruhusu kuwa mchezaji wa akiba katika michezo hiyo.
“Gabi amekuwa akijisukuma kila siku. Alikuwa anawaambia watu wote, ‘Nitarudi mapema, mapema, mapema,’ na amefanikiwa,” – Arteta alisema.

Arsenal wamemsajili tena Jesus kwenye orodha ya wachezaji wake wa Ligi ya Mabingwa Ulaya kuchukua nafasi ya Max Dowman, ambaye akiwa na miaka 15 alikua mchezaji mdogo zaidi kuwahi kucheza Champions League baada ya kuingia dakika za mwisho kwenye ushindi wa 3-0 dhidi ya Slavia Prague mwezi uliopita. Hata hivyo, Dowman alipata jeraha la kifundo cha mguu akiwa na timu ya under-21 Jumamosi.
“Kwa hiyo, kutokana na kazi ya Gabi na kazi yote ambayo timu ya matabibu imefanya kwa miezi hii, tuliweza kufanya mabadiliko hayo na tumeyafanya. Unamuona Max na hali yake, lakini pia unamuona Gabi na furaha yake kurudi katika Champions League,” – Arteta alisema.




