Jamila: Kwa Asec Mimosas lazima kieleweke

ISMAILIA: MSHAMBULIAJI wa JKT Queens FC, Jamila Rajabu, amesema wamejipanga kuyageuza mapungufu yao yaliyopita kuwa mabao katika mchezo wa pili hatua ya makundi dhidi ya Asec Mimosa ya Ivory Coast Ligi ya Mabingwa Afrika inayoendelea katika jiji la Ismailia, Misri.
Mchezo wa kwanza dhidi ya Gaborone United walitoka sare ya bao 1-1.
Jamila, ambaye aling’ara kwa kuwa mfungaji bora wa mashindano ya CECAFA yaliyofanyika Nairobi, Kenya, amesema leo kuwa mchezo wao wa kwanza dhidi ya Gaborone United ulionesha mapungufu katika eneo la mwisho la uamuzi, hali iliyochangia kutopatikana kwa bao licha ya nafasi kadhaa kuonekana.
Amesema benchi la ufundi tayari limefanyia kazi mapungufu hayo wakati wa mazoezi na sasa kikosi kipo kwenye hali nzuri ya ushindani na malengo makubwa ya kupata ushindi muhimu katika mchezo ujao.
“Tumerekebisha tulipokosea, safari hii nafasi zitageuzwa kuwa mabao,” amesema Jamila.
Mshambuliaji huyo mwenye kasi na ustadi wa kumalizia, ameongeza kuwa mechi za kiwango cha kimataifa zinahitaji umakini na nidhamu ya kiufundi kwa dakika zote, na ndicho wachezaji wa JKT Queens wamejipanga kukifanya wanapovaana na miamba hiyo kutoka Ivory Coast.
JKT Queens FC inatarajia kushuka dimbani Novemba 12, 2025 saa 12:00 jioni kwa saa za Misri, sawa na saa 1:00 jioni kwa saa za Tanzania, ikiwavaa Asec Mimosa katika mchezo unaotajwa kuwa wa kuamua nafasi nzuri katika kundi lao.




