Kwingineko

Inzaghi akimbilia mabilioni ya Waarabu

RIYADH: ALIYEKUWA kocha mkuu wa wanafainali wa Ligi ya Mabingwa Ulaya Inter Milan, Simone Inzaghi ametambulishwa rasmi kocha mkuu wa Al-Hilal ya Saudi Arabia siku moja baada ya kuondoka Inter Milan na wiki mbili kabla ya mchezo wa kwanza wa klabu hiyo ya Saudi Arabia kwenye Kombe la Dunia la Klabu, huku  ushawishi wa fedha wa warabu hao ukitajwa kuwa ni moja ya sababu za uamuzi huo wa Inzaghi.

Inzaghi, Mtaalamu wa soka la Italia amesaini mkataba wa miaka miwili baada ya Al-Hilal kumuwekea mezani ofa nono ya zaidi ya euro milioni 20 ambazo ni sawa na shilingi za kitanzania Bilioni 61.16 kwa msimu huku akianza kazi kwenye kombe la Dunia la Klabu ambalo Al Hilal ni washiriki.

Inzaghi mwenye miaka 49 aliachia ngazi baada ya Inter kunyooshwa mabao 5-0 na Paris Saint-Germain katika fainali ya Ligi ya Mabingwa Jumamosi iliyopita, ikiweka rekodi ya kuwa kipigo kikubwa zaidi katika historia ya miaka 70 ya fainali kubwa za Ulaya.

Kocha Inzaghi amelikalia benchi la ufundi la Inter kwa miaka minne akiiongoza klabu hiyo kutwaa taji la Serie A mwaka jana na pia aliiongoza Nerazzurri ilipopoteza taji la Ligi ya Mabingwa 2023 kwa mbele ya vigogo Manchester City.

Klabu yake mpya ya Al-Hilal itafungua dimba la Kombe la Dunia la Klabu dhidi ya Real Madrid Juni 18 kwenye Uga wa Hard Rock jijini Miami Gardens.

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button