Inspector Haroun kufanya kazi na Jux

DAR ES SALAAM:MSANII wa muziki anayefahamika kwa jina la Haroun Rashid ‘Inspector Haroun Babu’ ameweka wazi matarajio yake ya kuendelea kufanya kazi na wasanii mbalimbali wanaofanya vizuri katika muziki wa Bongo Fleva kwa sasa.
Akizungumza na SpotiLeo, Inspector Haroun Babu amesema tayari ana miradi kadhaa ya muziki inayoendelea, huku mingine ikiwa tayari imekamilika. Miongoni mwa wasanii anaotarajia kufanya nao kazi ni Country Boy, G Nako na Jux.
Aidha, msanii huyo amezungumzia tetesi zinazodai kuhusishwa kwake na kampeni mbalimbali, ikiwemo zinazohusu wasanii kuachana au masuala ya kisiasa.Ameweka wazi kuwa hahusiki na kampeni yoyote ya aina hiyo na hana uhusiano wowote na chama chochote cha siasa.
“Sijihusishi na siasa kwa namna yoyote ile, sina chama wala kampeni yoyote,” amesisitiza Inspector Haroun Babu.
Katika hatua nyingine, amekanusha madai ya kuwa anajiandaa kuacha muziki, akieleza kuwa bado ana hamu kubwa na anaona muziki bado unamdai.
“Sina mipango ya kuacha muziki kwa sababu bado naona muziki unanihitaji,” amesema.
Kuhusu uwezo wake wa kufanya maonesho ya moja kwa moja jukwaani, Inspector Haroun Babu amesema ana uwezo wa kuimba nyimbo zake zote ‘LIVE’.Ameeleza kuwa aina ya uimbaji hutegemea mahitaji ya mratibu wa tukio husika, kama anahitaji live performance au ‘playback’ ya kawaida.




