Ligi Kuu

Ibenge: Uwanja ulituzuia kucheza Vizuri

MWANZA: KOCHA Mkuu wa Azam FC, Florent Ibenge, amesema sare ya mabao 2-2 dhidi ya Pamba FC si matokeo mabaya, licha ya kukiri timu yake kuanza vibaya kutokana na Uwanja.

Akizungumza baada ya mchezo huo uliochezwa jana, Ibenge amesema walianza kwa presha kubwa kutokana na mazingira ya uwanja ambayo hayakuruhusu timu yake kucheza soka lao la kawaida.

“Hatukuanza vizuri kabisa mchezo huu. Uwanja haukuwa mzuri na hilo lilituathiri kwa kiasi kikubwa. Ilitubidi kucheza mipira ya juu na katika mipira ya kugombania walikuwa bora zaidi,” amesema Ibenge.

Kocha huyo amesema kuwa timu yake ilionesha unyonge katika dakika za mwanzo na kushindwa kumudu kasi ya wapinzani, hali iliyosababisha kuruhusu bao la kwanza. Baada ya hapo, benchi la ufundi lilibadilisha mbinu na kuamua kucheza soka la moja kwa moja (direct football) badala ya mtindo wao wa pasi nyingi.

Alikiri kuwa mabadiliko hayo yalileta nafuu na kuifanya timu ionekane bora zaidi, lakini makosa mwanzoni mwa kipindi cha pili yaliwagarimu tena kwa kuruhusu bao la pili.

Hata hivyo, Ibenge amesema kuingiza washambuliaji wawili kuliongeza nguvu eneo la ushambuliaji na kuwasaidia kurejea mchezoni hadi kusawazisha mabao.

Azam FC inakabiliwa na mchezo mwingine mbele yao utakaochezwa Alhamisi Machi 5 dhidi ya Tanzania Prisons kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya.

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button