Nyumbani

Hersi: ACA ni nguzo ya maendeleo ya michezo Afrika

DAR ES SALAAM: MWENYEKITI wa African Clubs Association (ACA), Hersi Said, amesema changamoto nyingi zinazokabili taasisi na klabu barani Afrika zinatokana na ukosefu wa umoja na sauti ya pamoja, hali inayochelewesha upatikanaji wa suluhisho la kudumu kwa masuala kama usafiri na uratibu wa shughuli za kimataifa.

Akizungumza Dar es Salaam, amesema lengo la ACA ni kujenga umoja huo muhimu ili taasisi zishirikiane kwa ufanisi zaidi katika kukabiliana na matatizo yanayojitokeza mara kwa mara, hasa yale yanayohusu gharama kubwa za usafiri kwa klabu na wachezaji.

“Umoja utatupa nafasi ya kujenga mifumo na mahusiano yenye manufaa, ikiwemo kupata punguzo la gharama kupitia mashirika ya ndege kama Air Tanzania, jambo litakalorahisisha safari za makundi makubwa kama timu na wanachama wetu,” amesema Hersi.

Ameongeza kuwa kupitia umoja huo, ACA inalenga kuboresha mifumo ya kisasa ya uanachama, masoko, udhamini, maendeleo ya vijana na uratibu wa shughuli za uhamisho wa wachezaji, ili kuinua hadhi ya michezo barani Afrika.

“Umoja unaleta heshima na uratibu bora. Kwa mfano, timu kama Yanga ikisafiri kwenda Malawi ikiwa chini ya mwamvuli wa umoja huu, inapokelewa kwa staha na urahisi zaidi kuliko mtu binafsi ambaye anaweza kukumbana na changamoto mbalimbali,” amesisitiza.

Kwa mujibu wa Hersi, ACA itaendelea kushirikiana na mashirika ya kimataifa na serikali za nchi wanachama ili kuimarisha mfumo wa ushirikiano wa klabu na wadau wa michezo kwa ustawi wa bara la Afrika.

Related Articles

Back to top button