Ligi Daraja La KwanzaMuziki

Halima apigwa nyundo miaka 3, faini milioni 3

DAR ES SALAAM: BARAZA la Sanaa la Taifa (BASATA) limetangaza kumfungia msanii Halima Haji kujihusisha na shughuli za sanaa kwa kipindi cha miaka mitatu, kufuatia kukiuka maadili katika kazi zake za kisanii.

Katika taarifa rasmi iliyotolewa na BASATA, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Leonidas Tibanga, imeelezwa kuwa uamuzi huo umefikiwa baada ya kusambaa kwa kipande cha video ya muziki ambacho hakikuzingatia maadili ya Mtanzania.

Baraza hilo lilifanya tathmini ya utetezi wa msanii huyo na kujiridhisha kuwa alitenda makosa ya kimaadili kwa makusudi.

Aidha, BASATA imebaini kuwa Halima Haji amekuwa akijihusisha na kazi za sanaa bila kusajiliwa rasmi na baraza hilo pamoja na kukosa kibali hai, jambo ambalo ni kinyume na taratibu za uendeshaji wa shughuli za sanaa nchini.

Kutokana na makosa hayo, BASATA imetoa maagizo matatu kwa msanii huyo. Kwanza, amepigwa marufuku kujihusisha na shughuli zozote za sanaa kwa muda wa miaka mitatu kuanzia tarehe ya uamuzi huo.

Pili, ametakiwa kushusha mara moja kipande hicho cha video kutoka kwenye mitandao na majukwaa yote ya kidijitali. Tatu, ametozwa faini ya shilingi milioni tatu (Tsh 3,000,000), ambayo anatakiwa kuilipa ndani ya siku 14 tangu tarehe ya kupokea taarifa hiyo.

Kwa mujibu wa BASATA, adhabu hiyo imetolewa kutokana na kusambaza maudhui yenye lugha ya matusi pamoja na maneno yanayodhalilisha heshima ya mwimbaji, msikilizaji na mtazamaji.

Related Articles

Back to top button