Kwingineko

Haaland awaka Norway ikiifumua Estonia 4-1

OSLO: KIUNGO wa Timu ya Taifa ya Norway Morten Thorsby amesema mawaidha ya nahodha wao Erling Haaland wakati wa mapumziko iliamsha ari ya timu na kuisaidia Norway kuifunga Estonia mabao 4-1, ushindi uliowaweka karibu na nafasi ya kufuzu Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza tangu 1998.

Haaland, aliyekuwa na kitambaa cha unahodha kufuatia kukosekana kwa Martin Odegaard ambaye ni majeruhi, aliwatuliza wachezaji baada ya kipindi cha kwanza kilichomalizika bila mabao jijini Oslo, huku mashabiki wenye hasira wakipiga kelele za kuwazomea walipoingia vyumbani.

Norway ilirudi kwa nguvu na kufunga mabao manne ndani ya dakika 12. Alexander Sorloth alifunga mawili mwanzoni mwa kipindi cha pili kabla Haaland kuweka kambani mabao yake mawili. Robi Saarma aliifungia Estonia bao la kufutia machozi dakika ya 64.

“Erling alikuwa mtulivu, akatupa Imani ‘Tutarekebisha hili, vijana. Tutapata bao, endeleeni kupambana.’ Hiyo ndiyo aina ya kujiamini tunayohitaji kwenye mechi kama hizi,” – Thorsby aliambia NRK.


Beki Torbjorn Lysaker Heggem alisema Haaland, ambaye sasa amefikisha mabao 53 ya rekodi ya Norway, pia alitoa ujumbe wa wazi wa kimbinu wakati wa mapumziko.

“Alituambia tumpelekee krosi zaidi tuingize mipira mingi kwenye boksi. Kwa kuwa walikuwa wanacheza chini sana, tulipaswa kuzunguka nao sana. Ilikuwa wazi kuwa ilifanya kazi baada ya dakika tano tu.” – aliongeza

Thorsby aliongeza kuwa Haaland na Odegaard wamepiga hatua kubwa sana kama viongozi na sasa wanaikumbatia zaidi nafasi yao kikosini.

“Wameanza kuelewa zaidi ushawishi walionao. Wanachokisema, wanachofanya na jinsi wanavyojituma huenea kwa wengine,” alisema.

Norway sasa wako mbioni kufuzu, wakiongoza Kundi I kwa pengo la pointi tatu dhidi ya Italia wanaoshika nafasi ya pili, ambao watasafiri hadi Oslo Jumapili. Italia huenda wakaambulia playoff ya mwezi Machi mwakani, kwani wana kazi ngumu ya kushinda Norway na kupindua tofauti ya mabao 17 jambo ambalo halionekani kuwezekana.

Related Articles

Back to top button