MWIGIZAJI anayefanya vizuri Tanzania akiwa anaigiza tamthilia ya Jua Kali, Godliver Gordian, amewataka wasanii pamoja na watayarishaji wa filamu kuwa na nidhamu ya kazi ili waweze kutimiza malengo yao na kufanya kazi zao kuwa nzuri na bora.
Gordian, ambaye alitwaa tuzo ya mwigizaji bora wa kike Tanzania mwaka 2021, ameweka wazi kuwa nidhamu ndio imekuwa msingi wa kila kitu kwenye jambo lolote lile.
Amesema kuwa licha ya kuwa na nidhamu kwenye kazi pia wasanii wanapaswa kuwa na upendo na Mungu na watu wengine kwani nidhamu na upendo ni vitu vinavyoenda sambamba katika kufanikisha mipango uliyojiwekea.
“Hii ni kwa wote walioko ndani ya sanaa ya uigizaji, nidhamu na Mungu vinapaswa kuwekwa mbele pindi unapotaka kufanya kazi yako, ni vitu viwili ambavyo vikiwa pamoja vinaleta uwiano wa kazi,” amesema Gordian.
Alisema kuwa iwapo utatanguliza hivi vitu viwili msanii lazima utafanya kazi yako vizuri na utafanikiwa lakini pia utaaminika na jamii inayokuzunguka na utaongeza wigo wa mashabiki wako.




