Filamu

George Folsey Jr. afariki dunia

LOS ANGELES: MHARIRI na mtayarishaji mkongwe wa Filamu huko Hollywood, George Folsey Jr., anayejulikana katika filamu na video mbalimbali ikiwemo video ya wimbo wa ‘Thriller’ wa hayati Michael Jackson, amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 85.

Mtoto wa mkongwe huyo, Ryan George, amethibitisha habari hiyo kwenye mitandao ya kijamii.

George Folsey Jr alifuata nyayo za babake, George Folsey Sr ambaye alikuwa muigizaji maarufu wa sinema aliyeteuliwa mara 13 kuwania tuzo za Oscar kutokana na filamu ya ‘Meet Me in St. Louis’ na ‘Seven Brides for Seven Brothers’.

George alianza kazi yake ya uhariri katika televisheni, akifanya kazi kwenye kipindi cha The Monkees mwaka 1967. Baadae aliingia katika kuangazia filamu akiwa katika mradi wa Black Caesar (1973).

Folsey Jr. alihariri filamu muhimu ikiwemo ‘National Lampoon’s Animal House (1978)’, ‘The Blues Brothers (1980)’, na video ya muziki ya Thriller isiyosahaulika (1983)’. Pia aliwahi kuwa mtayarishaji kwenye An American Werewolf huko London (1981), Trading Places (1983), na Spies Like Us (1985).

Kazi yake na Eddie Murphy ya Coming to Amerika (1988) inasalia kuwa moja ya mafanikio yake maarufu, akionesha ustadi wake katika kuchekesha, kuandika na kusimulia hadithi.

George alihusika katika ajali mbaya ya Twilight Zone: The Movie mnamo 1982, ambapo alipata ajali ya helikopta wakati walipokuwa wakipiga picha za filamu yao. Ajali hiyo ilisababisha vifo vya wagizaji watatu Vic Morrow na Watoto wawili ambapo walishitakiwa kuua bila kukusudia lakini baadae waliondolewa mashitaka hayo.

Licha ya changamoto hizo George aliendelea kufanya kazi kwenye miradi mikubwa. Alihariri filamu ya ‘Cheaper by the Dozen (2003)’, ‘The Pink Panther (2006)’, na ‘Hot Tub Time Machine (2010)’.

Mbali na kuhariri, George Jr pia alitoa filamu kama A Thing Called Love (1993) na Grumpier Old Men (1995). Kazi yake ya mwisho iliyopewa sifa ilikuwa kwenye tamthilia ya ‘Indie Summer Rain (2024).

Mchango wa George Folsey Jr kwenye sinema na video za muziki zinazofafanua utamaduni wa pop, umeacha alama isiyoweza kufutika huko Hollywood. Utaalamu wake, maono ya ubunifu na kujitolea kwake katika kusimulia hadithi kutakumbukwa kwa vizazi vijavyo.

Related Articles

Back to top button