Fabio avunja rekodi, avuka mechi 1300

RIO DE JANEIRO: KIPA wa Fluminense, Fabio amevunja rekodi ya muda mrefu ya golikipa Muingereza Peter Shilton ya kucheza mechi nyingi za ushindani katika soka la wanaume baada ya kucheza mechi yake ya 1,391 wakati timu yake ikishinda 2-0 dhidi ya America de Cali usiku wa Jumanne.
Mbrazil huyo mwenye umri wa miaka 44 amecheza soka la kulipwa kwa miaka 28, akicheza mechi yake ya kwanza ya ligi kuu akiwa na klabu ya Uniao Bandeirante aliyoichezea mechi 30, Vasco da Gama mechi 150, Cruzeiro mechi 976 na Fluminense alikocheza 235.
Alitoka Cruzeiro kwenda Fluminense mwaka 2022 na tangu wakati huo ameshinda taji moja moja la Recopa Sudamericanna na Copa Libertadores pamoja na mataji mawili mawili ya Taca Guanabara na Campeonato Carioca.

“Nina kila sababu ya kumshukuru Mungu kwa kuniwezesha kupata wakati huu maalum na kufikia hatua hii kubwa. Ilinifurahisha sana kuweka rekodi hii, haswa nikiwa na familia kando yangu. Ni furaha kubwa kufikia rekodi hii nikiwa ndani jezi ya Fluminense, ambayo ilinifungulia milango.” – Fabio alisema katika taarifa iliyotolewa na Fluminense.
Fluminense ilisherehekea rekodi ya Fabio kwa heshima katika Uwanja wa Maracana mjini Rio de Janeiro kufuatia ushindi wao mbele ya klabu ya América de Cali katika mkondo wa pili wa hatua ya 16 bora ya Copa Sudamericanna.
Kipa wa zamani wa England Shilton aliyecheza kati ya 1966 na 1997 alikuwa akishikilia rekodi ya michezo mingi zaidi ya soka la kulipwa japo jumla ya mechi alizocheza bado ni kitendawili rekodi zikisema mechi 1,390 wakati shilton mwenyewe akisema 1,387.




