Kwingineko

Donnarumma: Tuna njaa ya mafanikio

CALIFORNIA: Kipa wa mabingwa wa ulaya Paris Saint-Germain (PSG), Gianluigi Donnarumma ameonya kuwa mabingwa hao wapya wa Ulaya wana njaa ya mafanikio zaidi katika Kombe la Dunia la Klabu na wapinzani wao wasiwachukulie poa wakati huu wakijiandaa kukabiliana na Botafogo ya Brazil.

Donnarumma raia wa Italia aliwaambia waandishi wa habari kabla ya mechi hiyo ya leo Alhamisi kwenye Uwanja wa Rose Bowl kuwa kila mtu kwenye timu hiyo analikodolea macho taji hilo ili kukamilisha taji la tano msimu huu baada ya kuanza mashindano hayo kama walivyomaliza Ligi ya Mabingwa Ulaya.

“Kombe la Dunia la Klabu ni shindano muhimu sana kwetu, lazima tuendelee kuweka ‘focus’ yetu hapa tena kwa kwa asilimia 100 ili tufike fainali na tubebe hili kombe, Kila mtu kwenye kikosi ana njaa ya ushindi, kushinda mataji, na kufanikiwa ni muhimu kwa sasa na kwa mwaka ujao wa mashindano,” – alisema

Miamba hiyo ya Ufaransa walianza kampeni yao ya Kundi B kwa nguvu na kasi Jumapili, wakiizaba Atletico Madrid mabao 4-0. Ushindi huo ulikuwa ni ishara tosha ya namna walivyojipanga kwa shindano hili ikiwa ni zaidi ya wiki mbili tangu wawacharaze 5-0 Inter Milan katika fainali ya Uefa Champions League.

Wapinzani wa PSG, Botafogo walitinga Kombe la Dunia la Klabu kwa kushinda Copa Libertadores kwa mara ya kwanza mwaka 2024. Timu hiyo ya Brazil haikuingia kinyonge ilifungua kampeni kwa ushindi wa 2-1 dhidi ya Seattle Sounders Jumapili. Baada ya mchezo dhidi ya Botafogo, PSG itasafiri kaskazini hadi Seattle kwa mechi yao ya mwisho ya kundi dhidi ya Sounders Jumatatu.

Related Articles

Back to top button