Debora aapa kulipa kisasi kwa Asia

DAR ES SALAAM: BONDIA wa ngumi za kulipwa kutoka Tanzania, Debora Mwenda, ameahidi kulipiza kisasi dhidi ya mpinzani wake Asia Meshack katika pambano linalosubiriwa kwa hamu la Dar Boxing Derby litakalofanyika Julai 26, 2025, jijini Dar es Salaam.
Debora, anayefahamika kwa ukakamavu wake ulingoni, amesema bado anahisi maumivu ya kushindwa kwenye pambano la awali dhidi ya Asia, jambo ambalo limempa motisha ya kufanya maandalizi ya kina kwa ajili ya pambano hilo.
“Bado nina hasira ya kupoteza pambano hilo na nililia. Sasa hizo hasira zote zitamwangukia yeye. Mtarajie pambano kali, nimejifunza na nitapindua meza. Awamu hii lazima apate kipigo,” alisema Debora kwa kujiamini.
Bondia huyo amesema tayari ameingia kambini na anapitia programu ngumu ya mazoezi pamoja na mbinu mpya za kimchezo, akisisitiza kuwa Asia anapaswa kujiandaa kwa kipigo cha kitaalamu.
Kwa upande wake, bondia mwenzake Egine Kayange, amesisitiza kuwa pambano hilo ni zaidi ya mchezo, ni vita ya kisasi na heshima.
“Debora ni mpiganaji halisi. Sio kama Filbert Bayi akimbie vilima anabaki vitani hadi mwisho. Kauli yetu ni moja: ni akili nyingi. Asia anaujua moto wetu,” alisema Kayange kwa msisitizo.
Pambano hili linalojulikana kama Samia Calling Fight limevuta hisia za mashabiki wengi wa ngumi nchini, huku likitarajiwa kuwa moja ya mapambano yenye mvuto mkubwa katika kalenda ya mchezo huo kwa mwaka huu.
Mashabiki sasa wanasubiri kwa hamu kuona kama Debora ataweza kufuta machozi ya ushindi uliomponyoka awali na kuandika ukurasa mpya katika safari yake ya ndoto za ubingwa.