DC Ulanga aandaa tamasha
MKUU wa Wilaya ya Ulanga, Ngolo Malenya ameandaa tamasha la ‘Ulanga Iherepa’ kwa ajili ya kuhamasisha utalii wa ndani ili kuvutia wawekezaji katika sekta ya madini na utalii wilayani humo.
Iherepa ni neno la asili ya watu wa Ulanga lenye maana ya inayovutia, ‘Ulanga inayovutia’.
Akizungumza katika uzinduzi wa tamasha hilo juzi jijini Dar es Salaam, Malenya alisema limepangwa kufanyika Oktoba 22 na 23 ambapo kutakuwa na maonesho ya madini yanayopatikana Ulanga, maonesho ya utalii na kilimo pamoja na jukwaa kwa ajili ya wawekezaji.
Alisema katika tamasha hilo kutakuwa na mashindano ya mbio za miguu pamoja na mbio za baiskeli za milimani, washiriki pia watatembelea Hifadhi ya Taifa ya Nyerere kwa ajili ya kufanya utalii wa kupiga picha na utalii wa kuvua samaki ambapo ukishamvua samaki unamrudisha majini aondoke.
“Lakini pia kutakuwa na onesho la upigaji wa ngoma ya asili ambayo ni kubwa kuliko ngoma za kawaida, hii ilikuwapo toka ukoloni kwa ajili ya kudumisha mila. Ni ngoma maalumu inayopigwa kwa wakati maalumu, wanadai ukipitiliza muda ardhi inatikisika na sisi tutaomba wapitilize ili tuone,” alisema.
Alisema katika Jukwaa la Madini, wazawa watashirikiana na wawekezaji kutoka nje nchi na kuingia mikataba itakayosimamiwa na wizara husika sababu madini yanahitaji uwekezaji mkubwa na vifaa vya kisasa.
Alisema hadi sasa wawekezaji kutoka nje ni wengi wameshajitokeza, hivyo ikifika karibu na muda wa tamasha watajua ni wangapi kwakuwa kila siku maombi yanaongezeka kwaajili ya kutaka kuhudhuria tamasha hilo.




