
DAR ES SALAAM: MREMBO anayetikisa anga la muziki wa Bongo Fleva, Dayna Nyange, hatimaye amevunja ukimya wake na kuweka wazi maisha yake ya mapenzi, baada ya tetesi nyingi kusambaa mitandaoni.
Daina amewathibitishia mashabiki kuwa yupo kwenye penzi zito, ambalo wengi wameanza kuliita “penzi kilo 150”, baada ya kuchapisha picha mpya akiwa na mpenzi wake kupitia ukurasa wake wa Instagram.
Kupitia picha hiyo, mrembo huyo aliambatanisha ujumbe mzito wa mapenzi uliojaa hisia, akieleza namna alivyokuwa akionekana mchaguzi, lakini ukweli ni kwamba alikuwa anajua anachokitaka.

“Watu walikuwa wakiniambia mimi ni mchaguzi sana, na niliwaambia mimi si mchaguzi, najua tu ninachotaka. Leo nimewaambia nimekupata. Wewe ndiye ninayemtaka, wewe ndiye niliyemwombea. Wewe ni amani yangu. Wewe ndiye jibu la maombi yangu. Ninakuchagua wewe leo, kesho na milele. Nakupenda leo, kesho na siku zote,” ameandika Dayna.
Ujumbe huo umeibua hisia mseto mitandaoni, ambapo mashabiki na mastaa mbalimbali wamempongeza kwa hatua hiyo, huku wengine wakimtakia heri katika safari yake mpya ya mapenzi.
Je, huu ndio mwanzo wa ukurasa mpya wa maisha ya Dayna Nyange? Muda ndio utakaosema. Wapo wanaodai huenda ujumbe huo unaashiria wimbo mpya, huku wengine wakiamini ni kweli mpenzi wake ameoneshwa rasmi kwa mara ya kwanza.




