Chikola: Sijaja Yanga ‘kuuza sura’

DAR ES SALAAM: MCHEZAJI mpya wa Klabu ya Yanga, Offen Chikola, amesema amevutiwa sana na mapenzi makubwa ya mashabiki wa timu hiyo maarufu kwa jina la Wananchi, akisema ndio sababu kubwa iliyomfanya atamani kujiunga na timu hiyo.
Akizungumza kwa hisia kali katika mahojiano na klabu hiyo, Chikola amesema aliwahi kushuhudia namna mashabiki wa Yanga walivyomshangilia licha ya timu yao kupoteza mchezo dhidi ya timu aliyokuwa akiichezea wakati huo.
“Wananchi ni watu wa tofauti kabisa, wanapenda sana timu yao. Nakumbuka mechi tuliyocheza pale Dar es Salaam, Yanga walipoteza, lakini bado mashabiki walinishangilia binafsi kwa kile nilichokifanya uwanjani,” alisema Chikola aliyejiunga na Yanga akitokea Tabora United.
Mchezaji huyo ambaye anacheza nafasi ya ulinzi amesema tukio hilo lilimfundisha kuwa mashabiki wa Yanga ni watu wanaopenda soka la kweli, wanaojua kuthamini juhudi za mchezaji hata pale timu inaposhindwa.
“Toka siku hiyo nikajifunza kuwa hawa ni watu wa mpira. Ndiyo maana leo nipo hapa kama kijana wao. Nimekuja kufanya kazi, sijaja kutembea,” alisema kwa msisitizo.
Chikola amesema tayari ameanza kuhisi mapokezi mazuri kutoka kwa mashabiki wa Yanga na kuahidi kuonesha uwezo wake.
“Naomba ushirikiano wenu. Najua mmeshaanza kunipa moyo, nami nitaweka jitihada zote kuonesha kile nilichonacho mara tu nitakapopata nafasi ya kuaminiwa,” aliongeza.
Yanga imekuwa ikifanya usajili wa wachezaji mahiri katika maandalizi ya msimu mpya wa Ligi Kuu ya NBC na michuano ya kimataifa, huku Chikola akitajwa kuwa miongoni mwa nguzo muhimu katika safu ya ulinzi ya timu hiyo.




