Chelsea yawa ngazi ya Flamengo

PHILADELPHIA, Vigogo wa soka kutoka Brazil Flamengo imekuwa timu ya kwanza kufuzu hatua ya 16 bora ya kombe la dunia la Klabu linaloendelea nchini Marekani baada ya kupindua matokeo ya kipindi cha kwanza na kuwalaza Chelsea 3-1 kwa mabao ya kipindi cha pili kutoka kwa Bruno Henrique, Danilo, na Wallace Yan kuipatia timu hiyo ya Brazil ushindi wa pili mfululizo kwenye michuano hiyo.
Bao la mapema la Pedro Neto liliipa Chelsea uongozi dakika 13 tu kipindi cha kwanza lakini timu hiyo bingwa wa Conference League ilipoteza nafasi nyingi za kuendelea kutanua uongozi wao, na kuruhusu Flamengo kurejea tena mchezoni.
Wabrazil hao walifunga mabao mawili haraka haraka kupitia kwa Henrique na Danilo, dakika ya 62 na 65, mabao ambayo yalifuatiwa na tukio la mshambuliaji wa Chelsea, Nicolas Jackson, kuoneshwa kadi nyekundu ya moja kwa moja kwa rafu mbaya aliyocheza Katika harakati za kuwania mpira dakika tatu baadaye.
Flamengo walihitimisha karamu ya ushindi kwa bao la tatu la mshambuliaji wao Wallace Yan katika dakika ya 83 bao ambalo lilizima kabisa ndoto za Chelsea kupata angalau pointi moja kwa kulazimisha sare katika mchezo huo wa kundi D.
Matokeo hayo yanaifanya Flamengo kufuzu moja kwa moja wakiwa kileleni mwa Kundi D kwa pointi sita zilizotokana na ushindi katika mechi mbili za mwanzo.
Hatma ya Chelsea kusonga mbele kwenye michuano hiyo inatua mikononi mwa wababe wa soka kutoka Afrika Esperance de Tunis ambao wamepata pointi tatu kutoka kwa Wamarekani Los Angeles FC watakapo kutana Saa 10 alfajiri ya Jumatano ya juni 25.