Chana ataka mwongozo sanaa mtaa kwa mtaa

Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Balozi Dkt. Pindi Chana ameliagiza Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) kuandaa mwongozo wa kutekeleza programu ya sanaa mtaa kwa mtaa ili kuibua vipaji vingi kuanzia ngazi ya chini.
Kwa mujibu wa wizara hiyo Chana ametoa agizo hilo leo alipofanya ziara katika Baraza hilo ambapo amesisitiza Sekta ya Sanaa kuendelea kuongeza ukuaji katika Pato la Taifa.
“Natoa rai kwenu BASATA kuwa na takwimu sahihi kuhusu idadi ya Wasanii katika aina zote za Sanaa ambazo zitakuwa zinahuishwa kila baada ya muda mfupi na zitasaidia katika upatikanaji wa mikopo pamoja na udhamini kutoka taasisi mbalimbali,” amesisitiza Chana.
Akimkaribisha Waziri, Naibu Waziri wa wizara hiyo, Pauline Gekul amesisitiza Baraza hilo kutoa kipaumbele katika sanaa nyingine kama linavyofanya katika muziki pamoja na kutoa fursa kwa vikundi mbalimbali vya maeneo tofauti kushiriki matamasha ya kimataifa.