Bellingham kukosa mechi za kufuzu Euro 2024
KIUNGO wa Borussia Dortmund Jude Bellingham huenda akakosa michezo ya England ya kufuzu fainali za Euro 2024 mwezi Juni huku hofu ikizidi ya kufanyiwa upasuaji kutibu msuli wa goti.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 19 ndiye kiungo bora wa kizazi chake na amepata tuzo kwa kuwa na msimu wa mafanikio baada ya kutangazwa mchezaji bora wa mwaka wa Bundesliga kutokana na kuisaidia Borussia Dortmund kukaribia kutwaa ubingwa.
Bellingham amekuwa akicheza kwa miezi kadhaa akiwa amevaa bandeji kubwa kuzunguka mguu wake wa kushoto lakini pia mwisho wa wiki iliyopita ameonekana akiwa na bandeji ya aina hiyo kwenye mguu wake wa kulia.
Kikosi cha kocha Gareth Southgate kitakusanyika mwisho wa wiki hii kwenye kambi ya George Park, England kujiandaa kuzikabili Malta Juni 16 kabla ya kuikabirisha Macedonia ya Kaskazini Juni 19.




