Mastaa

BASATA yazindua “Rising Star Award” kukuza vipaji vya muziki nchini

DAR ES SALAAM: BARAZA la Sanaa la Taifa (BASATA) limezindua rasmi programu mpya ya BASATA Rising Star Award, jukwaa maalumu litakalolenga kuibua na kukuza vipaji vya wanamuziki chipukizi nchini.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo jijini Dar es Salaam, Katibu Mtendaji wa BASATA, Kelvin Stansilausi, amesema hii ni hatua muhimu katika safari ya kuimarisha sekta ya muziki Tanzania. Amesema kupitia jukwaa hilo, vipaji vipya vitapata nafasi ya kuonekana na kushindana si tu ndani ya nchi, bali hata kimataifa.

Programu hiyo imeandaliwa kwa ushirikiano na Alliance Française pamoja na Ubalozi wa Ufaransa nchini Tanzania, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kukuza uchumi wa ubunifu na kufungua milango ya kimataifa kwa wasanii wa Tanzania.

Kwa mujibu wa BASATA, Rising Star Award inalenga kutambua na kukuza wanamuziki chipukizi, kuwapa mwonekano mpana kupitia vyombo vya habari na kuwajengea uwezo kitaaluma kupitia mafunzo maalum. Washindi pia watapata fursa ya kutumbuiza kwenye majukwaa makubwa na kuandaliwa kushindana katika soko la kitaifa na kimataifa.

Mwakilishi wa BASATA Kimataifa, Flora Rousseau, amesema mshiriki atalazimika kuwa amesajiliwa BASATA na kuwa na namba halali ya usajili. Amefafanua kuwa programu inalenga wanamuziki ambao tayari wana nyimbo kwenye majukwaa ya kidijitali lakini wanakosa fursa ya matangazo na usimamizi wa kitaalamu.

Kwa upande wake, Lilian Shayo amesema BASATA ina mihimili mitatu mikuu ambayo ni Muziki, Maonyesho na Ngoma, na kwamba Rising Star Award ni sehemu ya mkakati wa kuendeleza muziki nchini.

Tuzo hizo zitahusisha mitindo mbalimbali ya muziki ikiwemo Bongo Flava, Hip Hop, Singeli, Reggae, Dancehall, Gospel, Amapiano, RnB pamoja na Folk na mitindo mingine ya kisasa, ili kuhakikisha ubunifu mpana unapata nafasi.

Kwa ujumla, uzinduzi wa BASATA Rising Star Award unaonekana kuwa mwanzo wa safari mpya ya kuibua kizazi kipya cha wasanii wenye ushindani wa kimataifa huku ukiimarisha usajili na weledi katika tasnia ya muziki Tanzania.

Related Articles

Back to top button