Muziki

Basata yamuonya Oscar, yampa muongozo

DAR ES SALAAM: KATIBU Mtendaji wa Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA), Dk. Kedmon Mapana, amemuonya msanii Oscar Oscar kuhusu wimbo wake Niombee na kumtaka azingatie maadili katika kazi zake za sanaa.

Baada ya kuachia wimbo huo siku chache zilizopita, BASATA ilimwita msanii huyo kufika ofisini kwao kufuatia malalamiko kutoka kwa baadhi ya wadau waliodai kuwa baadhi ya maneno katika wimbo huo hayana maadili. Leo Oscar alifika BASATA na kupewa mwongozo maalum wa kufuata.

Dk. Mapana amesema baraza limemkabidhi rasmi kitabu cha Mwongozo wa Maadili katika Kazi za Sanaa ili kimsaidie kuwa makini zaidi katika kazi zake zijazo.

Akizungumza na waandishi wa habari leo, Dk Mapana amesema wimbo wa Oscar hautaruhusiwa kupigwa asubuhi wala mchana, bali kuanzia saa sita usiku na kwa hadhira ya watu wenye umri wa miaka 18 na kuendelea.

“Tumemwambia Oscar kuwa wimbo wake unapaswa kusikilizwa na watu wazima tu na utaruhusiwa kupigwa redioni kuanzia saa sita usiku. Hautapigwa kwenye maeneo ya wazi kama vile mabasi au kwenye matamasha,” amesema Dk. Mapana.

Aidha, amewakumbusha wasanii wote nchini kutumia kitabu hicho cha mwongozo kama rejea ya kila siku katika shughuli zao, kwani ni nyenzo muhimu ya kukuza na kuimarisha tasnia ya sanaa kwa misingi ya weledi na maadili.

Kwa upande wake, Oscar amesema ameitwa nyumbani na yeye ametii kwa moyo mmoja na anaamini sasa ametambulika rasmi kama msanii.

“Kama hujawahi kuitwa BASATA, hujawahi kuwa msanii. Nimeitwa nyumbani na kuanzia sasa chochote nitakachokifanya lazima kipitie kule,” amesema Oscar.

Ameongeza kuwa yeye si chipukizi bali ni msanii anayejitambua na yuko tayari kufuata utaratibu uliowekwa kwa maslahi ya sanaa ya Tanzania

Related Articles

Back to top button