Kwingineko

Barcelona yatinga robo fainali kwa kishindo

BARCELONA, Hispania: KLABU ya FC Barcelona imeonesha ubora barani Ulaya baada ya kuichapa Newcastle United mabao 7-2 katika mchezo wa marudiano wa hatua ya 16 bora ya UEFA Champions League uliopigwa katika dimba la Spotify Camp Nou.

Ushindi huo mkubwa uliifanya Barcelona kusonga mbele kwa jumla ya mabao 8-3, ikiweka wazi dhamira yake ya kutwaa taji la michuano hiyo msimu huu.

Nyota wa mchezo huo alikuwa Raphinha aliyefunga mabao mawili na kutoa pasi mbili za mabao (assists), akiongoza safu ya ushambuliaji iliyokuwa hatari muda wote wa mchezo.

Barcelona ilianza kwa kasi baada ya Raphinha kufunga bao la mapema dakika ya sita kufuatia shambulizi la kushtukiza lililoanzishwa na Fermin Lopez. Hata hivyo, Newcastle walijibu kupitia Anthony Elanga aliyesawazisha dakika ya 15.

Kijana Marc Bernal aliirejesha Barcelona mbele kabla ya Elanga kufunga tena na kufanya mchezo kuwa sare ya 2-2 ndani ya dakika 30 za mwanzo.

Dakika za nyongeza za kipindi cha kwanza zilishuhudia Lamine Yamal akiifungia Barcelona kwa mkwaju wa penalti baada ya VAR kubaini faulo iliyofanywa na Kieran Trippier.

Kipindi cha pili kiligeuka kuwa maonesho ya nguvu kwa Barcelona, ambapo Fermin aliongeza bao la nne kabla ya Robert Lewandowski kufunga mabao mawili mfululizo, moja kwa kichwa na lingine baada ya pasi ya Yamal.

Raphinha alihitimisha karamu ya mabao dakika ya 73 akitumia makosa ya safu ya ulinzi ya Newcastle.

Licha ya ushindi huo mkubwa, Barcelona bado inaonekana kuwa na mapungufu katika safu ya ulinzi, kwani imefungwa mabao 17 katika mechi 10 za michuano hiyo msimu huu bila kupata ‘clean sheet’ hata moja.

Katika hatua ya robo fainali, Barcelona itakutana na mshindi kati ya Atletico Madrid au Tottenham Hotspur.

 

Related Articles

Back to top button