Baba Levo kuokota milioni 100 kwa Wakazi

DAR ES SALAAM: MBUNGE wa Jimbo la Kigoma Mjini, na Msanii Clayton Revocatus Chiponda ‘Baba levo,, ametangaza kuwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam imemhukumu msanii wa hip hop, Wakazi, kumlipa fidia ya Shilingi milioni 100 kufuatia kusambaza taarifa za uongo na za kashfa dhidi yake.
Kupitia mitandao yake ya kijamii, Babalevo amesema uamuzi huo umetolewa baada ya yeye kuwasilisha malalamiko mahakamani akidai kuwa Wakazi alimsingizia kwa kumhusisha na wizi wa simu za watu nchini Marekani, jambo lililochafua heshima yake.
“Leo Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imemuhukumu msanii Wakazi kunilipa milioni 100. Nadhani mnakumbuka nilipopoteza begi la simu Uturuki, Wakazi alisimama kutangaza kama nimeiba simu za watu Marekani.
Mbaya zaidi alianza kuyataja makampuni ninayofanyanayo kazi kuonesha yanafanya kazi na mwizi,” ameandika Babalevo.
Ameongeza kuwa licha ya kutopenda masuala ya kushitakiana mahakamani, alilazimika kuchukua hatua hiyo ili kulinda heshima yake.
“Kwangu mimi si jambo zuri kushitakiana mahakamani, lakini tunapaswa kutoshadadia mambo ya uongo kwa lengo la kumchafua mtu,” ameongeza.
Katika hukumu iliyotolewa Machi 13, 2026 na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, mahakama imebaini kuwa taarifa zilizotolewa na Wakazi zilikuwa za uongo, za kashfa na zenye madhara, ambazo ziliharibu sifa na heshima ya Babalevo katika biashara na tasnia ya muziki ndani na nje ya Tanzania.
Kutokana na uamuzi huo, mahakama imeamuru mambo yafuatayo:Wakazi atoe radhi hadharani kupitia vyombo vilevile vilivyotumika kusambaza taarifa hizo.
Amlipe Babalevo fidia ya Shilingi milioni 100 kwa madhara yaliyosababishwa.
Taarifa zote za uongo ziondolewe mara moja kwenye tovuti, mitandao ya kijamii, blogu, magazeti na chaneli za YouTube.
Mshtakiwa azuiwe kabisa kusambaza tena taarifa za uongo au za kashfa dhidi ya mlalamikaji.
Kiasi hicho cha fedha kitatozwa riba ya asilimia 7 kwa mwaka kuanzia tarehe ya hukumu hadi malipo yatakapokamilika.
Gharama zote za kesi zitalipwa na mshtakiwa.
Uamuzi huo umetolewa na mahakama ya Hakimu mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam na kuhitimisha rasmi shauri hilo kwa kumpa ushindi mlalamikaji, Babalevo.




