Azam FC yaelekeza jicho michuano ya Mapinduzi

DAR ES SALAAM: AZAM FC ni miongoni mwa timu zinazotarajia kushiriki michuano ya Kombe la Mapinduzi Zanzibar msimu huu baada ya kueleza mipango yake ya kujiandaa na mashindano hayo.
Timu hiyo inayowakilisha nchi kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho imesema inatarajia kuweka kambi Desemba 29, 2025 Visiwani Zanzibar ikiwa ni sehemu ya mpango mkakati wa kujiweka vizuri kabla ya mashindano kuanza mapema Januari.
“Mbele yetu kuna mashindano ya Mapinduzi, kwa sasa Ibenge na kikosi chake wako mapumziko hadi Desemba 23 watarejea kambini kwa maandalizi mafupi kisha tutaenda kambi Zanzibar kujiandaa na Kombe la Mapinduzi,”alisema.
Amesema lengo la kambi hiyo ni kuhakikisha timu inaingia kwenye Mapinduzi Cup ikiwa imara zaidi na yenye ushindani mkubwa, ikizingatiwa mashindano hayo hutumika kama kipimo cha pili cha maandalizi kuelekea kurejea kwa ligi mara baada ya AFCON.
Kipindi hiki timu nyingi zipo kwenye mapumziko kupisha fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON), mashindano ambayo huwahusisha wachezaji wengi wanaocheza katika ligi mbalimbali barani.
Ibwe ameongeza kuwa benchi la ufundi litajikita zaidi kwenye mazoezi ya ufundi na mbinu, sambamba na kuwapa nafasi baadhi ya wachezaji ambao hawajapata dakika nyingi katika michezo ya ligi, ili kuongeza ushindani na upana wa kikosi.
Michuano hiyo kwa msimu huu itatangazwa kesho na timu zilizothibitisha kushiriki huku wenyeji wa mashindano hayo wakisema awamu huu kuna timu nyingi kubwa kutoka mataifa mbalimbali.




