Arsenal yashusha ‘fundi’ mwingine

LONDON: Washika mitutu wa jiji la London Arsenal wametangaza kumsajili beki wa kati Cristhian Mosquera kutoka klabu ya Valencia inayoshiriki ligi kuu ya Spain LaLiga kwa mkataba wa muda mrefu.
Taarifa zaidi za uhamisho huo hazikufichuliwa lakini vyombo vya habari vya Uingereza vinaripoti Mhispania huyo mwenye miaka 21 amesaini mkataba wa miaka mitano kwa ada ya awali ya takriban euro milioni 15 pamoja na nyongeza.
Mosquera alihusika katika mechi 90 za Valencia kwenye michuano yote na alicheza mechi 37 kati ya 38 za LaLiga msimu uliopita na kuisaidia kumaliza nafasi ya 12. Beki huyo anaungana na Martin Zubimendi, Kepa Arrizabalaga, Christian Norgaard na Noni Madueke waliosajiliwa hivi karibuni.
Mshambuliaji Viktor Gyokeres pia anaripotiwa kukaribia kujiunga na klabu hiyo ya London huku meneja Mikel Arteta akipania kuimarisha kikosi chake baada ya kumaliza washindi wa pili katika misimu mitatu iliyopita ya EPL.
“Tunafuraha kumkaribisha Cristhian Arsenal. Akiwa beki mdogo na umri wa miaka 21, Cristhian tayari amefanya vyema mfululizo akiwa na uzoefu mkubwa wa kutoka LaLiga, Ni mchezaji mwenye akili na kasi nzuri, ambaye anaweza kucheza kati na pande zote mbili.” Arteta amenukuliwa na taarifa ya Arsenal.