Amorim awaomba radhi mashabiki United

GRIMSBY: MENEJA wa Manchester United Ruben Amorim ameomba radhi kwa mashabiki wa United baada ya kushindwa kupandisha kiwango cha klabu hiyo yenye historia kubwa duniani kilichopelekea kuondolewa kwenye raundi ya nne ya Kombe la Carabao na timu ya daraja la nne ya Grimsby Town usiku wa Jumatano.
Kwa dakika chache United walionekana kama wametoka gerezani kwenye uwanja wa Blundell Park wakati Harry Maguire aliposawazisha kwa kichwa dakika ya 89 na kufanya mambo kuwa 2-2 baada ya kutoka nyuma kwa mabao 2-0.
Ni kama Bahati haikuwa upande wao kwani hata mikwaju ya penalty 12 ilichagua kuzama kwenye nyavu zao zilizokuwa na ulinzi mkali wa Andre Onana na wao wakiweka 11 kwenye nyavu za Grimsby baada ya mchezaji mpya aliyesajiliwa majuzi Bryan Mbeumo, ambaye alikuwa anaanza vita kupambania namba United, mkwaju wake kungonga mwamba.
Alipotakiwa kueleza ni nini kilienda kombo, swali ambalo amelizoea tangu achukue hatamu za kuinoa United msimu uliopita, Mreno huyo hakusita na kujibu.
“Kila kitu, kwa jinsi tulivyoanza mchezo, ni kama hatukuwa hapa, wakati kila kitu kilichokuwa kikiendelea ni muhimu sana kwa klabu yetu, kila kitu kilichotokea, ni shida katika klabu yetu, tunapaswa kufanya vizuri zaidi. Lazima niwaombe radhi mashabiki wetu”.
“Haijalishi tumepotezaje. Hata katika mikwaju ya penalti, hisia ni zile zile. Nafikiri soka lilikuwa la haki leo. Timu bora imeshinda. Mimi ndiye meneja, kazi yangu inaapaswa kuwa kuelewa kilichotokea, na kwa mara nyingine tena nawaomba radhi sana mashabiki wetu, yaliyotokea ni zaidi ya matokeo. Tatizo kubwa katika timu lilikuwa wazi leo” – Amorim aliwaambia waandishi wa habari.
United imevuna pointi moja pekee kwenye mechi mbili za ufunguzi za Ligi Kuu ikiashiria mwanzo wa kuchechemea. Kuondolewa kwenye Carabao kunamaanisha matumaini ya kweli ya United kushinda kombe msimu huu sasa yamesalia kwenye Kombe la FA.