Habari Mpya

ALLY MAYAY TEMBELE>Tegemeo la maendeleo ya michezo nchini

Wanafunzi wa shule wa msingi na sekondari za KIbaha mkoan Pwani wakichuana katika mbio za meta 100 wakati wa tamasha la Michezo ya Olympi Africa la Michezo ya Vijana lililofanyika KIbaha. (Na Mpigapicha Wetu).

WADAU wa michezo nchini wameupokea kwa mikono miwili uteuzi wa mchambuzi wa michezo, Ally Mayay Tembele kuwa Kaimu Mkurugenzi wa Maendeleo ya Michezo nchini.

Mayay ambaye aliwahi kuwa mchezaji wa Yanga na nahodha wa timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, kwa miaka tofauti amechukua kijiti hicho kutoka kwa mtangulizi wake, Dk Yusuph Singo aliyepangiwa kazi nyingine.

MATUMAINI KIBAO

Wengi wa wadau wa michezo wameonesha matumaini na mwanamichezo huyo, ambaye kwa sasa ni maarufu kwa uchambuzi wa michezo na hasa soka katika televisheni.

SULEIMAN NYAMBUI

Kocha wa timu ya taifa ya riadha iliyoshiriki Michezo ya 22 ya Jumuiya ya Madola, Suleiman Nyambui amepongeza uteuzi wa Mayay, lakini amemuasa kutoangalia mchezo wa soka pekee kwa sababu ametoka huko.

Nyambui anasema kuwa Mayay kama anataka kufanya kazi zake vizuri na kuleta maendeleo ya michezo nchini, asiangalie mchezo wa soka pekee na badala yake awe mkurugenzi wa michezo yote.

Anasema watu wana mategemeo makubwa na Mayay, hasa ukizingatia kuwa michezo ilikuwa nyuma nchini kutokana na ukata, lakini sasa Serikali inazisaidia timu za taifa katika maandalizi na mashindano.

Nyambui ni miongoni mwa wanariadha wawili wa Tanzania waliowahi kutwaa medali katika Michezo ya Olimpiki baada ya kutwaa medali ya fedha katika mbio za meta 5,000 Moscow Urusi mwaka 1980.

FILBERT BAYI

Katibu Mkuu wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC), Filbert Bayi anasema Mayay ameteuliwa kutokana na ufahamu wake katika michezo, hivyo matarajio yake kuwa atafanya vizuri pamoja na kutokea katika soka kama hataingiliwa na wanasiasa.

Anasema kuwa binafsi anamwona Mayay kama Mkurugenzi wa Michezo tofauti na wengine waliomtangulia, kwani upeo wake ni mkubwa na anaweza kufika mbali, endapo atakuwa msikivu.

“Ally Mayay ni mwanamichezo, ameteuliwa kwa ufahamu wake katika michezo kwa ujumla pamoja na kwamba ametokea kwenye mpira, lakini anaweza kufanya vizuri kama hatayumbishwa na wanasiasa.

Binafsi, namwona kama Mkurugenzi wa Maendeleo ya Michezo tofauti na wengine waliotangulia. “Upeo wake katika mchezo wa mpira ni mkubwa, kwa kuwa atakuwa Mkurugenzi wa michezo na si wa mpira wa miguu na kama msomi atafanyia haki michezo mingine,” anasema Bayi.

BAKARI MALIMA

Mchezaji wa zamani wa Yanga na timu ya taifa, Taifa Stars, Bakari Malima au Jembe Ulaya alimpongeza Mayay kwa uteuzi huo na kusema tangu wakicheza wote Yanga na timu ya taifa, alikuwa na upeo mkubwa wa uongozi na alimtabiria kuwa kiongozi siku za baadaye.

Malima anasena ana matumaini makubwa na Mayay na atafanya vizuri na kutoa mchango mkubwa katika maendeleo ya michezo nchini.

ADEN RAGE

Mwenyekiti wa zamani wa Simba, Ismail Aden Rage anasema Mayay ana nidhamu na uwezo wa kuongoza, hivyo anampongeza Waziri Mchegerwa kwa uteuzi huo, kwani amewapa heshima kubwa.

“Namfahamu Mayay tangu akiwa kijana mdogo, ana nidhamu ya asili na waziri ametupa heshima kubwa, kwani huko nyuma waliteuliwa watu hata uwezo hawana,” anasema Rage. Anawaondoa hofu wadau wa michezo kutokuwa na hofu na Mayay, kwani ana uwezo mkubwa na anastahili nafasi hiyo.

SILAS ISANGI

Rais wa Shirikisho la Riadha Tanzania (RT), Silas Isangi anampongeza Mayay kwa kuteuliwa kushika nafasi hiyo kwani ni jambo zuri nafasi kubwa kama hiyo kushikwa na wanamichezo wenyewe.

Isangi anasema pamoja na Mayay kucheza soka na sasa kuwa mchambuzi wa mchezo huo, ana uhakika ataitendea haki na michezo mingine. Ni matarajio yake kuwa mkurugenzi huyo mpya wa michezo hatausahau mchezo wa riadha kwani ndio mchezo ulioliletea sifa kubwa taifa na unaendelea kufanya hivyo

Related Articles

Back to top button