Filamu

‘All’s Fair’ yaongezewa msimu wa Pili

NEW YORK: TAMTHILIA ya kisheria ya Kim Kardashian, ‘All’s Fair’, imeongezewa msimu wa pili baada ya kupata mafanikio makubwa katika siku zake za kwanza sehemu mbalimbali ilipooneshwa.

Kampuni ya uandaaji wa filamu ya Disney imeagiza msimu wa pili wa kipindi hicho cha Ryan Murphy ambacho pia kinawashirikisha Naomi Watts, Niecy Nash-Betts, Teyana Taylor, Matthew Noszka, Sarah Paulson na Glenn Close kutokana na kufanya vizuri zaidi kati ya tamthilia mpya za Hulu Original katika kipindi cha miaka mitatu, kulingana na takwimu za siku tatu za kwanza zilizotazamwa.

Kipindi hicho kilizinduliwa mapema mwezi huu, na tamati yake ya msimu wa kwanza yenye sehemu mbili inatarajiwa kurushwa Desemba 9 kimataifa kupitia huduma hiyo ya utiririshaji.

‘All’s Fair’, iliyoandikwa na kuzalishwa na Murphy, ambaye pia ndiye muongozaji, inaelezea kikundi cha mawakili wanawake wa talaka wanaoacha kampuni yao inayoongozwa na wanaume na kuanzisha kampuni yao binafsi.

Licha ya mafanikio yake ya kutazamwa, tamthilia hiyo imepokea ukosoaji mkali kutoka kwa wachambuzi wa filamu. Kwa sasa, All’s Fair ina asilimia 3 pekee kwenye kipimo cha Tomatometer cha Rotten Tomatoes, kinachopima mapendekezo ya wakosoaji wa kitaalamu.

Hata hivyo, kwa upande wa hadhira, tamthilia hiyo imepata asilimia 66 kwenye Popcornmeter, kipimo kinachotokana na maoni ya watazamaji.

Glenn Close, mmoja wa waigizaji wakuu, amekuwa akipigia debe ubora wa kipindi hicho, akisema tayari ameangalia msimu mzima na kukipatia sifa kubwa.
Akihojiwa na gazeti la The Guardian, Close alisema:
“Nakuapia Mungu, nimeona sehemu zote tisa na ni nzuri ajabu… Ni tamthilia ya kusisimua, inayovutia na wakati mwingine kuhuzunisha.”

Muigizaji huyo mkongwe pia alimsifia Kim Kardashian kuwa mchapakazi mzuri na mwenye akili nyingi.
Alifichua kuwa wakati wa kurekodi tamthilia hiyo, Kim alikuwa akijiandaa kukamilisha masomo yake ya sheria na mara nyingi alikuwa na makaratasi ya kujisomea (flashcards) wakati wa mapumziko.

“Ni mtu mzuri sana, mwenye akili na anayejali sana watoto wake. Alikuwa akisoma kwa bidii ili kumaliza shahada yake ya sheria. Nilimuuliza kama ataitumia, akasema, ‘La, nataka tu kuihifadhi kama akiba.’”

Related Articles

Back to top button