Kwingineko

Ajax yasaka tena heshima yake ulaya

AMSTERDAM: Vigogo wa Ligi Kuu ya Uholanzi maarufu Eredivisie Ajax Amsterdam wanaukaribia ubingwa wa ligi hiyo na kupindua hadithi mbaya walioanza nayo misimu miwili iliyopita nayo mwanzo wa msimu baada ya kupata moto katika kipindi hiki ligi hiyo ikielekea ukingoni.

Ajax wana uongozi wa pointi tisa mbele ya PSV Eindhoven walio katika nafasi ya pili, zikiwa zimesalia raundi tano kabla ya msimu huu wa Eredivisie kumalizika, mwisho utakaoifanya Ajax kuwa kwenye mbio za kurejesha makali yake na kuweka rekodi kwa kutwaa taji lake la 37.

Ajax wanahitaji pointi saba kati ya 15 kutoka kwenye mechi zao 5 zijazo ili kurejesha makali yake kwenye soka la Uholanzi. Wanaweza kutwaa taji hilo mapema Aprili 27 watakapowakaribisha Sparta Rotterdam lakini wanahitaji kwanza kushinda ugenini dhidi ya Utrecht iliyo nafasi ya nne Jumapili hii na kuwaombea mabaya PSV ikiwa wanataka kuandaa sherehe za ubingwa nyumbani.

Akili kubwa na mpango wa kocha Francesco Farioli, mwenye miaka 34, mwanzoni mwa msimu unaonekana kuzaa matunda huku akirudisha touch ya asili ya Ajax, akiweka kipaumbele kwenye ‘rotation’ ya wachezaji wake 39 anaowatumia msimu huu lengo likiwa ni kuboresha utimamu wa mwili na kuimarisha safu ya ulinzi.

Ingawa amelaumiwa kwa kutotumia mbinu ya asili ya Ajax maarufu kama ‘Total Football’, Ajax wameshinda mechi 13 kati ya 14 zilizopita za ligi na kuwapita mabingwa watetezi PSV katika mbio za ubingwa.

“Tumebakiwa na fainali tano za kucheza. Ulikuwa ushindi muhimu sana, bila shaka tumefanikiwa kumaliza katika nafasi tatu za juu. Hii ina maana kwamba tumefuzu kwa hatua ya awali ya Ligi ya Mabingwa, ambayo ni muhimu kwa klabu.” kocha Farioli alisema baada ya ushindi wa ugenini wikendi iliyopita dhidi ya Willem II.

Ajax ilitwaa taji hilo mara ya mwisho mwaka wa 2022, ambapo baada ya hapo kocha wao Erik ten Hag aliondoka kwenda Manchester United na wachezaji wengi muhimu waliuzwa, na hivyo kusababisha msukosuko ambao haujawahi kushuhudiwa kwa mabingwa hao wa zamani wa Ulaya.

Mrithi wa Ten Hag, Alfred Schreuder alianza vyema kwa ushindi kwenye sita mfululizo za ligi, lakini baadae kibao kiligeuka haraka na vipigo mfululizo vikafuata. Ajax ilicheza mechi saba mfululizo saba bila kushinda, ambayo ilimfanya Schreuder atimuliwe.

Kuanzia msimu uliopita wakiwa na Maurice Steijn ambaye hakutangazwa kama kocha mkuu, Ajax ilifufua matumaini ya kurejesha ufalme wao baada ya kutumia kiasi cha Euro milioni 100 (dola milioni 114) kuimarisha kikosi. Lakini baada ya miezi mitatu, kocha huyo mpya aliondoka wakajipata katika nafasi ya mwisho kwenye ligi ya Uholanzi kwa mara ya kwanza kwenye historia ya klabu.

Ajax ilifanyia kazi matatizo yake na kutafuta njia ya kujinasua lakini bado waliendelea kunyanyasika huku wakikikumbuka kipigo cha 6-0 kutoka kwa Feyenoord, na kumaliza msimu wa tano, pointi 35 nyuma ya mabingwa PSV. Ujio wa Farioli mwaka jana ulionekana kuwa hatari, lakini ujenzi wake wa kikosi umekuwa wa haraka na sasa klabu hiyo inatafuta heshima yake iliyopotea katika soka la ulaya.

Related Articles

Back to top button