Adele kujitenga na muziki kwa muda

LAS VEGAS, Marekani: MWANAMUZIKI wa Uingereza aliyetamba na wimbo wa ‘Hello’, Adele Laurie ameweka wazi kwamba kwa sasa hana mpango wa kutoa wimbo mpya kwa sababu anajiandaa kupumzika kufanya muziki kwa muda.
Nyota huyo mwenye miaka 36 yupo katika mapumziko kwenye makazi yake Las Vegas ambapo ataendelea kutumia muda mwingi akiwa na familia yake akiwemo mtoto wake wa miaka 11 Angelo.
Adele ambaye pia ana makazi nchini Ujerumani katika jiji la Munich alipoulizwa kuhusu kutoa wimbo mpya hivi karibuni alijibu kutokuwa na mpango wa kufanya hivyo kwa sasa.
“Nataka kupumzika nadhani nataka kufanya vitu vingine vya ubunifu, lakini pia natamani kupata mtoto mwingine,” Adele alieleza.
Hata hivyo Adele anayetamba pia na wimbo wa ‘I Set Fire To The Rain’ ni mshindi wa tuzo za Grammy, ameahidi atakaporejea katika muziki atarekodi nyimbo mpya na atafanya ziara ulimwenguni kote.
“Ukweli ni kwamba nimekuwa na albamu nne tu! Sidhani kama watu wengi wanajua hili. Pia sifahamu kama wanafahamu kuwa mtoto wangu ana miaka 11 ambaye ukipiga hesabu utagundua nilimpata nikiwa na miaka 21 na sasa nina miaka 36 natamani kuwa na mtoto mwingine,” alisema Adele.
Adele alijipatia umaarufu akiwa na miaka 19 na mwaka wa 2008 aliachia albamu yake ya kwanza, kabla ya kuachia albamu yake ya pili akiwa na miaka 21 mwaka 2011 na mwaka 2015 aliachia albamu yake ya tatu akiwa na umri wa miaka 25.
Albamu yake ya pili aliyoiachia mwaka 2011 ndiyo albamu ya nne iliyouzwa zaidi wakati wote nchini Uingereza, nyuma ya Malkia, ABBA, na The Beatles.
Mara ya mwisho kutumbuiza nchini Uingereza ilikuwa Julai 2022 kwenye Tamasha la Saa ya Majira ya Uingereza huko Hyde Park, London.