Mchekeshaji Eric Omondi kukimbilia Ikulu kwa mazungumzo

NAIROBI: MCHEKESHAJI wa Kenya, Eric Omondi ameweka wazi mpango wake wa kuzuru Ikulu ya Kenya siku ya alhamis hii ya Julai 11 mwaka huu akidai kupeleka ujumbe wa vijana wakiitaka serikali ibadilike.
Katika video inayoonyesha ujumbe wa Omondi inamuonyesha akiwa amevalia mavazi meupe huku ameshikilia bendera ya Kenya, aliwasilisha maombi ya dhati kwa Rais William Ruto akimtaka achukue hatua za haraka kujenga imani ya wananchi kwa serikali ikiwa ni pamoja na kuwafuta kazi Makatibu wa Mawaziri, Makatibu Wakuu na wakuu wa mashirika ya serikali wasioweza kumaliza changamoto za wakenya.
Omondi alitangaza maandamano ya amani hadi Ikulu mnamo Alhamisi saa 11 asubuhi. Alisisitiza kuwa hii ni fursa ya mazungumzo ya moja kwa moja, mbali na kelele za mitandao ya kijamii. Ujumbe wake utajumuisha wanawake 100, vijana 100 na wanaume 100 huku akisisitiza wote wavae mavazi meupe, kuashiria umoja na amani.
Katika ujumbe wake huo Omondi amewataka polisi kudumisha mtazamo usio na vurugu, akisisitiza umuhimu wa mazungumzo hayo ni ya kujenga.
Hatua hii inafuatia ibada ya hivi majuzi ya ukumbusho iliyoandaliwa na Jenerali Z ya kuwaenzi wenzake waliopoteza maisha wakati wa maandamano ya hivi majuzi.
Mchekeshaji Omondi amekuwa akitetea haki za vijana mara kwa mara, haswa kushiriki katika maandamano ya kupinga Mswada wa Fedha.