Nyumbani

Msheri, Kibwana mazungumzo yanaendelea Yanga

DAR ES SALAAM: GOLIKIPA Abtwarib Msheri na beki wa kulia Kibwana Shomari wamemaliza mikataba yao na wapo huru kujiunga na timu yoyote kama mazungumzo na timu waliyokuwa wakiitumikia ya Yanga hayatokamilika.

Msimamizi wa wachezaji hao, George Job amesema wachezaji hao wameshamaliza mikataba yao na bado wanaangalia ofa kutoka timu nyingine mbalimbali zilizoomba huduma yao ingawa mazungumzo na Yanga iliyoonyesha nia ya kuwabakiza wachezaji hao yakiendelea.

“Kwa sasa wachezaji hao Kibwana na Msheri wapo huru na wamepata ofa kutoka timu nyingi za ndani lakini Yanga wameonyesha nia ya kuwabakiza wachezaji hao na leo (jana) tulikuwa katika mazungumzo nao ingawa bado hayajakamilika,” ameeleza George Job.

Alisema mazungumzo hayo yalishindwa kufanyika mapema kwa sababu Yanga ilikuwa katika masuala ya kufungiwa kusajili wachezaji wandani na nje kutokana na madai ambayo hadi sasa wameshamalizana nayo na wapo huru kusajili ndiyo maana mazungumzo yameanza sasa.

George amesema kwa Msheri kwa sasa yupo mapumzikoni kwa kuwa muda baada ya wachezaji kupewa mapumziko yeye alikuwa na timu ya taifa kule Zambia lakini pia aliporudi aliendelea kucheza katika mabonanza mbalimbali ya mechi za hisani yaliyoandaliwa na wachezaji wenzake hivyo hakupata muda mzuri wa kupumzika kama wenzake.

“Tumepokea ofa na vilabu kadhaa lakini Yanga wameonyesha nia ya kuwabakiza Msheri na Kibwana ndiyo maana mazungumzo yameanza na katika orodha ya wachezaji wanaotaka kubaki Yanga nao wamo,” alimaliza George

Related Articles

Back to top button