Man United yataka mshambuliaji mpya
KOCHA wa Manchester United Erik ten Hag anataka kusajili mshambuliaji mpya katika dirisha la usajili la kiangazi.
Mholanzi huyo alihisi safu yake ya ushambuliaji ingempa mabao mengi zaidi ila imekuwa tofauti kwani hadi sasa United imefunga mabao 45 huku zikiwa zimebaki mechi saba ligi kumalizika.
Ten Hag aliongeza: “Unahitaji chaguo zaidi. Unahitaji nafasi mbili katika kila nafasi.
“Baadhi ya nafasi ambazo hatukuwa na chaguo msimu huu nafasi ya mshambuliaji, nafasi ya beki wa kushoto na hiyo ina athari mbaya kwa matokeo.”
United, ambao watasafiri kumenyana na Bournemouth leo, walimsajili fowadi wa Denmark Rasmus Hojlund kutoka Atalanta kwa £72m kwa mkataba wa miaka mitano Agosti mwaka jana.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 21 ndiye mfungaji bora wa klabu hiyo katika kampeni yake ya kwanza akiwa na mabao 13 katika mechi 34 alizocheza katika mashindano yote.